Rais Magufuli aiwezesha Serengeti Boys

Muktasari:

  • Wachezaji wa timu hiyo pamoja na benchi la ufundi limewatoa hofu Watanzania na kuahidi kutowaangusha katika fainali hizo na kucheza Kombe la Dunia kwa mashindano hayo.

RAIS wa Jamhuri ya Tanzania, John Magufuli ametoa kiasi cha Sh1 bilioni kwa ajili ya maandalizi ya fainali za Afrika (AFCON) zinazotarajiwa kufanyika nchini mwezi Aprili mwaka huu.

Rais Magufuli ametoa kiasi hicho cha pesa jana Jumatatu Ikulu wakati anatoa pongezi kwa timu ya Taifa Stars ambayo imefuzu kucheza fainali za Mataifa Afrika (AFCON) zitakazofanyika Juni mwaka huu Misri na bondia Hassan Mwakinyo ambaye alimpiga Sergio Eduardo Gonzalez.

Alisema, kiasi hicho cha pesa ni kwa ajili ya kuendesha mashindano hayo ambayo yatachezwa kati ya Aprili 14 na 28 kwenye viwanja viwili jijini Dar es Salaam, Taifa na Chamazi Complex.

Kutokana na imani aliyonayo Rais Magufuli kwa vijana wa Serengeti Boys aliwaambia wafanye vizuri na kufuzu kucheza Kombe la Dunia kwa mashindano hayo.

Wachezaji wa timu hiyo pamoja na benchi la ufundi limewatoa hofu Watanzania na kuahidi kutowaangusha katika fainali hizo na kucheza Kombe la Dunia kwa mashindano hayo.

Kocha wa makipa wa Taifa Stars, Manyika Peter amesema: “Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano hayo, alichokifanya Rais Magufuli ni hamasa nzuri kwa timu na wachezaji na uzuri imetoa mapema kilichobaki ni utekelezaji tu.” Kuhusu kucheza Kombe la Dunia, Manyika amesema hakuna kisichowezekana kwa sababu kila kitu ni mipango na uwajibikaji.

Katika fainali hizo Serengeti Boys imepangwa kucheza Kundi A kwenye mashindano hayo pamoja na timu za Angola, Uganda na Nigeria. Itafungua mashindano hayo na Nigeria.

Hii ni mara ya pili kwa Serengeti Boys kufuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza ilikuwa mwaka juzi na mashindano yalifanyika Gabon na sasa inaendelea na maandalizi ya mashindano hayo kwenye Uwanja wa JK Park jijini Dar es Salaam.