Rage: Milioni 30 ya JK nilizipeleka huku

Muktasari:

Rais Magufuli pia amewahi kutoa Sh 1 Bilioni kwa ajili ya kufanikisha mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana (Afcon) yaliyofanyika nchini ambapo Tanzania iliwakilishwa na timu ya Serengeti Boys, huku pia akiisaidia Taifa Stars katika kusaka tiketi ya kufuzu kushiriki Afcon.

Dar es Salaam.Siku chache baada ya rais Mstaafu, Jakaya Kikwete (JK) kueleza namna alivyotoa Sh 30 Milioni kwa ajili ya kununua uwanja wa Simba, aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage ameleza namna alivyopewa fedha hizo na alipozipeleka.

Rage amesema alimfuata Rais Kikwete baada ya kupungukiwa Sh30 Milioni  na alikubali kuisaidia klabu hiyo.

"Nilikuwa na Sh50 Milioni, tulipungukiwa Milioni30 nikamuomba rais Kikwete, tukiwa katika mkutano wa uongozi, alinipigia simu akasema Rage uliniomba fedha, njoo Ikulu," anasimulia Rage.

Anasema alikwenda Ikulu na kuwaacha wenzake katika mkutano, alipofika alikaribishwa na chai Ikulu akanywa kisha rais Kikwete akamkabidhi fedha hiyo.

"Nilirudi kwenye mkutano na kuikabidhi ile fedha kwa mweka hazina, utawala wa kina Aveva (Evance ambaye alikuja kuwa rais wa Simba) walichangia pia Sh 10 Milioni, tukanunua uwanja ule kwa Sh90 milioni," alisema n a kufafanua.

"Eneo hilo waliohusika kulitafuta ni Dalali (Hassan aliyekuwa mwenyekiti wa Simba kabla ya Rage) na Kaduguda (Mwina aliyekuwa katibu mkuu wa Simba.

Alisema fedha hiyo ilitumika kwenye ununuzi wa ujenzi wa uwanja wao kama ambavyo ilipangwa na si kwingine kokote.

"Utumie fedha ya rais kwa matumizi tofauti kweli! unajipenda au? ile fedha ilitumika kwenye ununuzi wa uwanja wetu," alisisitiza Rage.

Alisema rais Kikwete pamoja na kwamba amesema alitoa Sh 30 Milioni, lakini ameisaidia klabu ya Simba vitu vingi wakati wa utawala wake huku mfumo huo ukiendelea pia kwa mrithi wake, rais John Pombe Magufuli ambaye amesema pia amekuwa na mchango katika kusaidia michezo nchini.