Rage: Ligi Kuu Tanzania ifutwe, Simba apewe ubingwa

Muktasari:

Kauli ya Rage ya kutaka ligi ifutwe imekuja siku chache baada ya Makamu mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela kunukuliwa akitaka ligi ifutwe na ianze upya baada ya kuondoka kwa janga la corona.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa zamani ya Simba, Aden Ismail Rage amesema anatamani Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ifutwe na Simba ipewe ubingwa.

Ligi Kuu Tanzania imesisima kutokana na tishio la janga la ugonjwa wa corona linalotikisa dunia kwa sasa na hakuna muda wa mwisho unaojulikana kwa kurejea kwa ligi hiyo.

Kauli ya Rage ya kutaka ligi ifutwe imekuja siku chache baada ya Makamu mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela kunukuliwa akitaka ligi ifutwe na ianze upya baada ya kuondoka kwa janga la corona.

Rage alisema kutokana na janga hili la corona basi ligi ikifutwa waangalie msimamo anayeongoza awe bingwa, mengine yaendelee kwani Tanzania haitakuwa ya kwanza.

Katika hatua nyingine Rage amewataka wachezaji kuwa waangalifu wa kufanya mazoezi wakiwa majumbani.

Rage amesema mazoezi nyumbani kutaepusha maambukizi ya corona kwenda eneo ambalo wanakuwepo watu wengi sio sahihi.

"Tukizingatia amri ya serikali yakututaka tukae nyumbani, itasaidia janga hili kupita kwa haraka kwani kila mtu atajilinda kwake,"

Ameongeza kuwa "Kuhusu wachezaji kwenda viwanjani ama gym ambako kila mtu anakwenda wanapaswa kuwa waangalifu, lengo ni moja tu kuondoa kusambaza corona."