Rachier awachorea giza wanaopinga

Wednesday April 3 2019

 

By Thomas Matiko

Nairobi. UNAWEZA kusema Mwenyekiti wa Gor Mahia, Ambrose Rachier ameamua kuwachorea giza baadhi ya viongozi wenza katika klabu hiyo hasa wale wanaotofautiana naye sana kwenye masuala ya uongozi.

 Stori ipo hivi, Jumanne wiki ijayo, klabu hiyo itaaanda mkutano mkuu na wanachama wake ambapo ajenda kubwa itakuwa ni kufanyia mageuzi baadhi ya sheria za uongozi wa klabu hiyo.

 Sasa kwenye mabadiliko hayo yaliyopendekezwa kuidhinishwa kwenye kikao hicho, mengi yanaonekana kuwalenga viongozi wanaompinga Rachier huku zikionekana kumlinda yeye.

 Hata hivyo, kulingana na Rachier ambaye kama sheria hizo zikiidhinishwa, zitamwezesha kuongoza klabu hiyo kwa miaka mingine minane, hivyo kuhakikisha anahudumu kwenye wadhifa huo kwa zaidi ya miaka, mabadiliko hayo ni kwa ajili ya kuboresha utendakazi klabuni.

 Kulingana na mapendekezo ya sheria hizo mpya kwa mujibu wa Rachier ambaye ni wakili, ni kwamba, mtu yeyote atakayekuwa akiwania wadhifa wowote ndani ya Gor, ni lazima kiwango cha kisomo chake kisiwe chini ya diploma.

 Sheria hii, kama ikiidhinishwa na wadau, itaishia kumfungia nje Katibu Mtendaji, Judith Nyangi ambaye mara kwa mara kwa kipindi cha miaka minne iliyopita amekuwa akitofautiana sana na staili ya uongozi wa Rachier.

 Hata hivyo, pengine kwa kusoma ishara hizo, Nyangi ametangaza atakuwa akiwania wadhifa wa mweka hazina kwenye uchaguzi ujao wa klabu.

 Pendekezo lingine ni kwamba, kwa mwaniaji wa wadhifa wa Afisa Mkuu Mtendaji wa Klabu, lazima naye awe kahitimu na kumiliki angalau Shahada ya Biashara.

 Hii ina maana kwamba Afisa Mkuu Mtendaji wa sasa, Lordvic Aduda, naye huenda akashindwa kuwania wadhifa huo, kwa kuwa hajahitimu kwenye levo hiyo.

 Mabadiliko mengine ambayo yamependekezwa ni kwa Gor kufutilia mbali nyadhifa nane ikiwamo Naibu Mwenyekiti Mkuu, Naibu Mwenyekiti wa kwanza, Naibu Mwenyekiti wa pili, Naibu Katibu Mkuu, na ile ya Katibu Mkuu Msaidizi.

 Kama nyadhifa hizo zikifutiliwa mbali, basi viongozi watakaopigwa shoka ni George Wasuna, John Pesa, George Ongudi, Kevin Odhiambo na Ronald Ngala ambao sasa watalazimika kugombea nyadhifa nyinginezo.

Mapendekezo hayo hata hivyo yanapendekeza kuhifadhiwa kwa nyadhifa za Mwenyekiti, Naibu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, na Mweka Hazina.

 Aidha mapendekezo hayo yanasema kila mgombea wa nyadhifa yoyote ile, ataruhusiwa kugombea kwa mihula miwili tu ya miaka minne.

 Kwa maana hiyo, Rachier ambaye tayari ameiongoza Gor kwa kipindi cha miaka 12, atakuwa na fursa ya kupiga shughuli hiyo kwa miaka mingine minane zaidi.

Advertisement