Prisons yaitolea macho Singida United

Muktasari:

Timu ya Prisons imepania kushinda mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida United ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo.

Kocha wa Prisons, Abdallah Mohammed alisema ni muhimu kushinda mchezo huo, baada ya kupoteza mechi tano msimu huu.

Dar es Salaam. Kocha wa Prisons, Abdallah Mohammed amesema mchezo wa Jumamosi dhidi ya Singida United ni muhimu kushinda ili kurejesha morali ya kikosi chake.

Prisons inayotoka mkoani Mbeya, imecheza michezo tisa imeshinda mmoja, imetoka sare mitatu na imepoteza mitano katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Prisons imeshindwa kupata matokeo mazuri katika Ligi Kuu msimu huu, baada  ya kuondokewa na aliyekuwa mfungaji wake bora Mohammed Rashid aliyesajiliwa na Simba.

Kocha huyo alisema havutiwi na mwanzo mbaya katika mashindano hayo baada ya kufungwa michezo mitano inayoiweka Prisons katika mazingira magumu.

Mohammed aliyetwaa tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu msimu uliopita baada ya kuiwezesha Prisons kumaliza katika nafasi ya nne, alisema mchezo dhidi ya Singida utakuwa ni vita.

"Timu siyo mbaya ukiangalia tunacheza vizuri lakini hatupati ushindi, hilo ndilo tatizo letu linalotukabili kwa sasa.

 

"Tatizo liko katika safu ya ushambuliaji ambayo imekuwa butu.Hatufungi mabao yatakayoipa timu ushindi,” alisema Mohammed.

Alisema ana matumaini Prisons itaanza kupata matokeo mazuri, baada ya kufanyia kazi kasoro zilizochangia timu hiyo kutofanya vyema.