Polisi waiwekea mkakati Mbeya City

Muktasari:

Beki huyo licha ya kuwa msimu wake wa kwanza katika Ligi Kuu, lakini amekuwa na uhakika wa namba kikosini, huku akicheza mechi 27 hadi sasa.

Mwanza. Beki wa kati wa Polisi Tanzania, Mohammed Kassim amesema matokeo ya suluhu waliyopata Jumamosi dhidi ya Prisons, yametibua hesabu zao na sasa wanajipanga upya kusaka ushindi dhidi ya Mbeya City.

Kassim ambaye ni anacheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu, juzi alifikisha mchezo wake wa 27 kati ya 33 waliyocheza Polisi Tanzania na kuisaidia kuondoka na alama moja ugenini na kufikisha pointi 48 na kukaa nafasi ya sita.

Maafande hao baada ya mchezo wao wa juzi, wanatarajia kushuka tena uwanjani kesho Jumatano kukabiliana na Mbeya City, mchezo utakaopigwa dimba la Sokoine, huku wenyeji wakihitaji ushindi ili kujinasua nafasi za mkiani.

Kassim amesema malengo yao ilikuwa ni kuvuna pointi sita katika Jiji la Mbeya, lakini kwa matokeo ya juzi tayari wameshakwama hivyo wanaanza kusaka alama nne katika mechi hizo mbili.

Amesema katika mchezo huo walikutana na ushindani mkali kwani wapinzani walihitaji kutumia faida ya uwanja wao wa nyumbani kupata ushindi lakini hata wao walipambana kuondoka na alama moja.

"Bado malengo yetu hayajafikia kwa sababu tulilenga kuondoka Jijini Mbeya na pointi sita lakini tayari tumeshapoteza mbili hivyo tunajipanga kushinda dhidi ya Mbeya City ili kuchukua nne, " amesema Kinda huyo.

Ameleeza kuwa anaamini benchi la ufundi liliangalia mapungufu yaliyoonekana kuhakikisha wanayarekebisha ili mchezo ujao waweze kufanya kweli na kufikia malengo yao msimu huu katika kumaliza nafasi nne za juu.