Pogba anaondoka? Labda baadaye sana

Wednesday July 29 2020

 

MANCHESTER, ENGLAND. UNASUBIRI Paul Pogba aondoke? Utangoja sana unaambiwa.

Kiungo huyo Mfaransa ameshusha hofu mashabiki wa miamba hiyo ya Old Trafford ataendelea kuwapo kwenye kikosi, akifurahia kufuzu mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Mkali huyo anayesakwa na Real Madrid amekuwa moto tangu ligi iliporejea, huku ripoti zikidai mchezaji huyo ameshakubali kusaini dili jipya la miaka mitano ya kubaki kwenye kikosi hicho.

Baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Leicester City, ambapo umeifanya Man United kumaliza ligi kwenye nafasi ya tatu, Mfaransa huyo mshindi wa Kombe la Dunia, aliposti kwenye mitandao ya kijamii “Twenzetu Ligi ya Mabingwa mwana.”

Pogba amekuwa moto uwanjani tangu aliporejea uwanjani akitokea kwenye majeruhi, huku akitengeneza kombinesheni matata kwenye sehemu ya kiungo pamoja na fundi wa mpira Mreno, Bruno Fernandes aliyetua Old Trafford kwenye dirisha la usajili wa Januari.

Wakati huo huo, klabu za Real Madrid na Juventus zilizokuwa zikionyesha kumhitaji Pogba, nazo zimepunguza kasi yake - huku ikidaiwa jambo hilo linatokana na ukata uliosababishwa na janga la corona.

Advertisement

Kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer amekiri kufurahishwa na kiwango cha soka cha Pogba tangu aliporejea kutoka majeruhi huku ubora wake ukiisaidia timu hiyo kumaliza kwenye tatu bora ya Ligi Kuu England.

Kutokana na hilo la Pogba kubaki, kocha Solskjaer huenda sasa akaweka mkazo kwenye usajili wa beki wa kati na winga Jadon Sancho kuliko kuwekeza kwenye kiungo ya kati na kuna mastaa wengi wa nafasi hiyo waliopo kwa sasa Old Trafford.

Advertisement