Pochettino amtoka Wanyama kidesign

Tuesday August 27 2019

 

By Thomas Matiko

ENYEWE siku ya nyani kufa miti yote hutuleza. Hatma ya nahodha wa Harambee Stars, Victor Wanyama ndani ya Tottenham Hotspurs sasa ipo wazi baada ya Kocha Mauricio Pochettino kumtoka kidesign.

Pochettino kakiri waziwazi hamhitaji Wanyama  tena na hawezi kumpa namba kwa misingi ya ‘huruma’ ila tu kwa kuzingatia kiwango.

Tango msimu huu ulipoanza, Pochettino hajamtumia kabisa. Alimweka benchi kwenye mechi yao ya kwanza dhidi ya Aston Villa ila hakumtumia. Kwenye sare dhidi ya Manchester City na kichapo dhidi ya Newcastle, Pochettino alimchuja hadi kwenye benchi.

Hivi majuzi Pochettino akifunguka na Shirika la habari la AFP, alimgeuka Wanyama na kusema hana haja naye kwa sasa akisisitiza kiwango chake kimeshuka mno hivyo haoni vipi anaweza kuendelea kumhitaji.

“Victor ni mchezaji muhimu lakini kutokana na mambo kadha wa kadha karudi nyuma. Ninapokosa kumchezesha mchezaji ni kwa sababu katika mawazo yangu naamini yupo mwingine aliye kwenye ubora zaidi. Jukumu langu na benchi la ukufunzi ni kuwapanga wachezaji walio kwenye kiwango. Tunapanga kikosi kwa misingi ya ubora na wala sio huruma. Soka linahusu ubora wa kiwango cha  leo na kesho na wala sio jana,” Pochettino aliyemdhamini sana Wanyama kwenye msimu wa kwanza tangu alipomsajili, akasema.

Pochettino alikuwa akimwamini sana Wanyama na ndio sababu yake ya kumsajili kutoka Celtic ya Scotland na kumleta Uingereza kujiunga na Southampton.

Advertisement

Baada yake kuhamia Spurs 2016, alihakikisha tena kamsajili Wanyama. Hata hivyo, baada yake kung’aa kwenye msimu wa kwanza alipojiunga na Spurs, majeraha yakajongea na kumfanya kupoteza namnba na imani ya Pochettino ambaye sasa kakiri wazi wazi hana kazi tena naye.

Tetesi zinaarifu kuwa Club Brugge ya kule Ubelgiji tayari imeonyesha nia ya kumsajili kabla ya dirisha lao kufungwa Septemba mbili mwezi ujao.

Mpaka sasa majadiliano baina ya klabu hizo zinaendelea na kama dili hiyo itakosa kiufanikiwa, basi huenda Wanyama atalazimika kuendelea kukosa mechi hadi dirisha dogo la Januari litakapofunguliwa.

Hata hivyo, mmoja wa jamaa kutoka familia yake kafichua dili hiyo mpaka sasa imefanikiwa kwa asilimia 70%.

 Mkataba wa Wanyama na Spurs unaomlipa Pauni 65,000 (Sh8.1 milioni) kila wiki ungali na miaka miwili. Taarifa zinaarifu kinachosalia ni masuala ya mshahara wake na Club Brugge.

Advertisement