Pep, Jose washika shingo ya Ole

Muktasari:

Man United haijapata ushindi kwenye mechi tatu zilizopita, huku Kocha Ole akishinda mara nane tu tangu alipopewa mkataba wa kuwa kocha wa kudumu jambo linalowafanya mashabiki kuchukia kwa sababu ameifanya timu hiyo kuwa ya kawaida sana. Mashabiki hao wengi wanaamini Mauricio Pochettino atafaa kuwaondoa kwenye hali ngumu inayowakabili kwa sasa.

MANCHESTER, ENGLAND . MASHABIKI wa Manchester United wanamtaka Kocha Ole Gunnar Solskjaer afutwe kazi baada ya kushindwa kuwachapa Aston Villa uwanjani Old Trafford.

Mashabiki hao walichukizwa kwelikweli na Solskjaer baada ya matokeo ya 2-2 na hivyo kuwafanya kutumia kurasa zao wa mitandao ya kijamii kuwasilisha mawazo yao ya kumtaka kocha huyo aondolewe kwenye timu mara moja.

Man United haijapata ushindi kwenye mechi tatu zilizopita, huku Kocha Ole akishinda mara nane tu tangu alipopewa mkataba wa kuwa kocha wa kudumu jambo linalowafanya mashabiki kuchukia kwa sababu ameifanya timu hiyo kuwa ya kawaida sana. Mashabiki hao wengi wanaamini Mauricio Pochettino atafaa kuwaondoa kwenye hali ngumu inayowakabili kwa sasa. Shabiki mmoja aliandika: “Hebu fukuza huyu mpuuzi, kama yeye ni gwiji wa klabu hiyo haina maana hafukuzwi.”

Shabiki mwingine aliyetambulika kwa jina la @RedDevilBible aliandika: “Samahani sana hii haikubaliki. HAIKUBALIKI.” Mwingine, @wickedchandy aliandika: “Fukuza huyu Mnorway wa ovyo. Haeleweki, kuendelea kuwa na imani na kocha wa hivi, ambaye haonekani kama ataleta mafanikio ni upuuzi.”

Mwingine @AWBsTackle, aliandika: “Kushinda mechi 7 kati ya 33. Yani Thelathini na tatu. Hebu mwondoeni huyo mwalimu wa shule, mchukueni Poch.”

Hizo ni kelele za mashabiki wa Man United. Lakini, Kocha Solskjaer mwenyewe anapaswa kujitazama pia baada ya timu yake kufanya ovyo huku kukiwa na makocha kibao wa maana hawana kazi. Max Allegy, Pochettino na Unai Emery wapo tu mtaani hawana kazi.

Man United ipo nafasi ya tisa kwa sasa kwenye msimamo wa ligi, wakivuna pointi 18 katika mechi 14, ikiwani kiwango kibovu zaidi kuwahi kutokea kwenye timu hiyo baada ya miaka kibao. Kwenye mechi hizo, wameshinda nne tu, sare sita na vichapo vinne. Kwa mwendo huo, ambapo kwa sasa timu imecheza mechi tatu za mwisho bila ya ushindi, Solskjaer anajiweka kwenye wakati mgumu zaidi kama hatapata matokeo ya ushindi ndani ya mechi mbili au tatu zijazo.

Bahati mbaya zaidi kwa Old ni mechi mbili zijazo atakabiliana na Jose Mourinho uwanjani Old Trafford, kisha Pep Guardiola huko Etihad. Kwa kifupi tu, Mourinho na Guardiola ndio wanaoshikilia hatima ya Ole kwa sasa baada ya timu kufanya hivyo siku za karibuni. Man United ikichapwa na Tottenham uwanjani Old Trafford kisha ikaenda kukumbana na kipigo tena kwa Manchester City huko Etihad, bila ya shaka hadi kufikia hatua hiyo, Man United itakuwa imeporomoka kwenda chini zaidi kwenda kwenye msimamo wa ligi na hilo halitamwaacha salama Solskjaer. Baada ya hapo Man United itakipiga na AZ Alkmaar kwenye Europa League, Everton kwenye Ligi Kuu England na Colchester kwenye robo fainali ya Kombe la Ligi.