Paul Nonga : Mwamuzi wa mechi Lipuli aliyekimbia benchi Yanga

Muktasari:

Mkongwe huyo kwenye soka amethibitisha kuwa alianza kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2011 na aliingia mkataba wa miaka miwili na timu ya JKT Oljoro ya Arusha.

WAKATI Simba wakijivunia Meddie Kagere unaambiwa Lipuli FC huwaambii kitu kwa nahodha wao, Paul Nonga, ambaye ndiye amekuwa akiamua matokeo katika michezo ya Ligi Kuu Bara.

Kwa Simba asipofunga Kagere kuna Miraji Athuman, lakini mmoja ndiye baba lao na upande wa Lipuli FC basi kama sio Nonga ujue Deruweshi Salibobo atatia kitu kambani.

Kwa sasa Nonga anafukuzia anga za Kagere kwenye mbio za kuwania Kiatu cha Dhahabu msimu huu akiwa na mabao sita huku kinara (Kagere) akiwa na mabao saba.

Mkongwe huyo kwenye soka amethibitisha kuwa alianza kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2011 na aliingia mkataba wa miaka miwili na timu ya JKT Oljoro ya Arusha.

“Nilicheza misimu miwili baada ya kuonyesha uwezo mzuri nikawavutia matajiri wa Mbeya City ambao, walinisajili kwa mkataba wa miaka miwili,” anasema.

Baadaye akapata ulaji Mwadui FC na alishindwa kumaliza mwaka kutokana na kuwavutia mabosi wa Yanga.

“Nilikaa miezi sita nikasajiliwa na Yanga ambako pia sikudumu kwa muda mrefu kutokana na kukosa namba kikosi cha kwanza kitu ambacho hakikuwa kipaumbele changu.

“Yanga nilidumu kwa miezi sita nikaomba kuondoka sababu ya ushindani wa namba nikarudi Mwadui tena nikacheza misimu miwili 2016/2017 na 2017/2018.

“Baada kumaliza mkataba wangu na Mwadui nilijiunga na Lipuli FC msimu wa mwaka 2018/2019 na nikaongeza mpaka sasa 2019/2020. Nimecheza timu hizo zote kwa mafanikio isipokuwa Yanga sikupata namba kikosi cha kwanza,” anasema.

Nonga anafichua siri ya mafanikio yake, aliweka wazi kuwa ni kuamini katika upambanaji na kuheshimu kazi hiyo kama sehemu ya kujiingizia kipato.

“Soka ndio maisha yangu nalichukulia kama ajira, hivyo nipo tayari kucheza popote ili mradi napata maslahi na kazi yangu inaonekana. Mbali na maslahi, lakini jambo la msingi huwa naangalia mahali ambako napata muda wa kucheza mara kwa mara,” anasema.