Papy Tshishimbi: Usajili makini utaibeba Yanga

IMEBAKI kama wiki moja tu kabla ya kurejea tena uwanjani tangu michezo ilipositishwa nchini kwa sababu ya janga la virusi vya corona.

Kurejea tena kwa Ligi ni hatua ambayo kila mchezaji alikuwa akiitamani na sasa tunaomba Juni 13 ifike na kila mmoja kuvaa tena jezi ya klabu yake kisha kufanya kile kinachotakiwa na kusubiriwa na mashabiki.

Ligi Kuu Bara inarejea na mashabiki wanarudi tena kutupa nafasi ya kuwatumikia na ni wasaa mzuri kuweza kuwapa kile wanachotarajia kutoka kwetu.

Leo tumekutana tena katika ukurasa wangu na nitaendelea kubaki kwa klabu ya Yanga ambayo muda mfupi ujao itaingia katika fursa ya kusajili ili kuiboresha timu yetu tayari kwa msimu ujao.

Uongozi wetu una dhamira ya kufika mbali katika mafanikio, unatamani kuona msimu huu tunakata tiketi ya kushiriki mashindano ya Afrika mwakani, bado kuna ligi kuu ambako tunahitaji kupambana kushinda na kusubiri kuona walio juu wakianguka, pia tuna nafasi ya kukata tiketi hiyo katika Kombe la Shirikisho.

Tukimaliza hapo naamini viongozi wetu watakuwa na akili moja ya kuhakikisha wanaisuka timu yetu kwa kazi kubwa ya msimu ujao ambao utakuwa na umakini katika kuhakikisha malengo yanafikiwa.

Nasema hivi kwa sababu mimi kama nahodha wa Yanga nimekuwa nikikutana na vikao mbalimbali vya viongozi na hata wadhamini, lakini pia hata timu kwa ujumla

tumekuwa tukikumbushwa hayo.

Yanga itaingia katika usajili, hebu tujiulize, inatakiwa iingie vipi ili ifanikiwe kupata kile inachostahili kwa hadhi ya klabu yetu?

Jina kubwa la klabu ni hatua ya wazi itamvutia mchezaji yeyote wa kawaida au mkali kuja kuitumikia klabu yetu kwa malengo ya klabu na yake binafsi. Mchaguzi wa kwanza na wa mwisho anakuwa Yanga yenyewe kwa kuangalia mchezaji husika kumfuatilia kwa kina kisha kuzungumza naye hatimaye kukubaliana na kumalizana.

Kwa sasa naweza kuwa shuhuda mzuri na kukubaliana na viongozi kwamba, safari yetu msimu huu ilikuwa na changamoto ya ubora kwenye kikosi chetu.

Tulifanya usajili mkubwa kama huu ambao tunakwenda kuufanya, lakini baadaye mambo yakatokea juu ya ubora na mengine kisha tukajikuta tunapoteza yale tuliyopanga kuyafanya.

Nafasi hiyo inarudi tena, haitawavutia wanachama na mashabiki wa klabu katika kurejea yale ambayo yalitokea huko nyuma.

Hebu nishauri klabu yangu, niseme inatakiwa ifanye kipi. Kwanza Yanga ni kubwa kuliko mchezaji na katika hilo ndio inayotakiwa kuwa na msuli inapomfuata mchezaji inayemtaka.

Siku zote mchezaji ndio anatakiwa kuikimbilia timu pale inapomtaka ndio maana sio jambo geni kusikia Eden Hazard alikuwa na ndoto za kuichezea Real Madrid, lakini kiu ya Madrid itakuwa tofauti wao watakuwa na kiu ya kubwa ya kupata mchezaji bora kwa hadhi ya klabu yao.

Yanga inatakiwa kuwa na uchunguzi wa kina katika kufanya maamuzi ya kumchukua yeyote na kwa hadhi ya Yanga inatakiwa kupata kile kilicho bora kule anakotoka.

Kutofanyika umakini katika eneo hilo ndio chimbuko la kwanza klabu kuanza kupoteza fedha katika kusajili wachezaji ambao hawatakuja kuwa na hadhi ya kuvaa jezi ya klabu.

Makosa hayo hubainika mara baada ya mchezaji kufika Tanzania na kujiunga na klabu ambako mashabiki wataanza kuona ubora mdogo na baadaye mchezaji kushindwa kuhimili presha za mashabiki ambao huwa na matarajio makubwa kwao wanapojiunga na klabu zao.

Kupanuka huku kwa hasara, pia kutahamia kwa klabu kutamani kuvunja mikataba ambayo ni hatua ngumu zaidi ambayo ni wazi fedha zitakuwa zimepotea.

Mkataba wake utasitishwa ndani ya muda mfupi hasara hii inaweza kuepukika kama mambo yatafanyika kwa upana na kuwa na muda wa kutosha.

Sishangai kuona wachezaji wengi wakivumishwa kuja kujiunga na Yanga kwa kuwa huo ni uthibitisho kwamba Yanga ina hadhi kubwa kuizidi hadhi ya mchezaji.

Eneo lingine la kuangalia ni aina ya mikataba ambayo klabu inatoa kwa wachezaji, naiona klabu ikipata wakati mgumu katika uamuzi wa mikataba tangu nimefika hapa nimekuwa nikisikia mara nyingi wachezaji kupewa mikataba ya miaka miwili au chini yake yaani mwaka mmoja na wengine mpaka miezi sita. Hii mikataba ya namna hii haitoi nafasi kwa klabu kufurahia muda wa mkataba na mchezaji wake.

Naziona klabu zikitoa fedha nyingi na wakati mchezaji husika anataka kuanza kuonyesha ubora na hapo ndipo muda wake unaishia katika klabu yake.

Vurugu zinarudi tena kuanza maongezi na mbaya mazungumzo hayo mara nyingi huja wakati ligi inafikia ukingoni hatua ambayo klabu inakosa utulivu mzuri wa kuamua hatima ya mchezaji husika kwa afya bora.

Inawezekana wakati huu ukamnufaisha sana mchezaji lakini ni hasara kubwa kwa klabu kutokana na maamuzi yatakayofanyika kwani inawezekana yakawa yanatoka nje ya bajeti ambayo ilipangwa awali au kuwa ndani ya uwezo wa klabu.

Klabu inatakiwa kuwa na upana wa maamuzi ili kuipunguzia hasara kubwa. Inatakiwa kufanya maamuzi kwa wakati kuepusha migongano ya kimasilahi.