Panama yafunguka sababu za kuingia mitini

Thursday July 30 2020

 

By Mustafa Mtupa

BAADA ya kutofika uwanjani katika mchezo wake dhidi ya Ruvuma Queens uliokuwa upigwe Julai 22, 2020 katika Uwanja wa Majimaji, Songea katibu Mkuu wa Panama Girls, Satana Chonya amesema sababu kubwa iliyowafanya kutofika ni kukosa usafiri kwa sababu ya hali yao ya kiuchumi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Satana alisema walikutana na changamoto ambayo imesababishwa na hali yao ya kiuchumi ambayo sio nzuri kwa sasa.

"Shida ni za kawaida tu, tulikosa usafiri na tuliwasilisha maombi kwenda kwa TFF ili wasogeze mchezo huo mbele" alisema Satana kabla ya mchezo huo ambao Panama ilikubali kichapo cha aibu cha mabao 11-0 ulipopigwa Jumatatu Julai 27.

Mbali na hilo Mwanaspoti ilizungumza na Kapteni wa timu hiyo ambaye anacheza nafasi ya golikipa Judith Isack alisema kuwa wao kama wachezaji wanajaribu kupambana kuhakikisha wanaikomboa timu hiyo kwenye janga la kushuka daraja lakini hali ya mazingira ya timu inawaangusha.

“Kiukweli ni mazingira ndio yanatufelisha ukiangalia kuna michezo mengine hata kocha hayupo, tumecheza mechi mbili bila ya mwalimu, pia huwa wana badilika badilika, lakini pia ukiangalia wachezaji wengi waliopo kwenye timu ni vijana alafu hawakai na mwalimu kwa muda mrefu jambo linalo sababisha kutokua kiuchezaji,” alisema.

Kwa sasa timu hiyo inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi ya wanawake ikiwa na alama nne baada ya kucheza mechi 18.

Advertisement

Panama itakuwa na kibarua mbele ya Marsh Queens katika mchezo ambao utapigwa Uwanja wa Samora, mkoani Iringa 1, Agosti. Huku Ruvuma yenyewe itakuwa na shughuli pevu mbele ya Kigoma Sisterz katika Uwanja wa Majimaji saa 10:00 jioni tarehe hiyo hiyo.

Advertisement