Pamba walikosea hapa FDL

Muktasari:

Pamba yenye maskani yake jijini hapa ilibaki kwenye mashindano hayo baada ya kuwatandika Friends Rangers kwa ushindi wa jumla wa 2-1 kwenye mchezo wa hatua ya mtoano wa kubaki kwenye mashindano hayo.

UONGOZI wa Pamba FC umekiri wazi kuwa na kikosi cha wachezaji walioshuka kiwango, majeruhi wa mara kwa mara ndio sababu kubwa ya wao kufanya vibaya kwenye Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu uliopita.

Pamba yenye maskani yake jijini hapa ilibaki kwenye mashindano hayo baada ya kuwatandika Friends Rangers jumla ya mabao 2-1 kwenye mchezo wa hatua ya mtoano wa kubaki kwenye mashindano hayo.

Akizungumza na Mwanaspoti Online, Katibu wa klabu hiyo Johnson James amesema hawakuwa na kikosi bora kitu ambacho kilifanya washindwe kufanya vizuri kwenye ligi hiyo kundi B na kuponea kwenye hatua ya mtoano.

“Hatukuwa vizuri msimu uliopita na sababu kubwa ni kuwa na timu yenye wachezaji ambao viwango vyao vimeshuka na pia tulikuwa na majeruhi wengi ambao wa muda mrefu hivyo walishindwa kuisaidia timu.

"Tunataka msimu ujao tuwe na kikosi bora hivyo tutabaki na wachezaji sita pekee na tutakachokifanya tutasajili wengine wapya 21 ambao tunaamini watatusaidia kwenye mashindano hayo,” amesema James.

Amesema watakuwa makini kwenye usajili huo ambao watasajili nyota mbalimbali kutoka Ligi Kuu, FDL na Ligi Daraja la Pili (SDL) ambao watajiridhisha kwanza ubora wao kabla ya kuwasaini mikataba.

“Tumepata somo kubwa msimu uliopita hivyo, tutakuwa makini kwa kila jambo ambalo tutalifanya ikiwepo suala la usajili tunataka kuwa na kikosi bora msimu ujao,” amesema Katibu huyo.