Ozil atoswa Arsenal apewa ofa nyingine

Saturday October 24 2020
ozil pic

LONDON, ENGLAND. FUNDI wa mpira, Mesut Ozil amepewa ofa ya kwenda kuwa mchambuzi kwenye studio za televisheni ya BT Sport baada ya Mjerumani huyo kufichua kwamba alitumia muda wake kuitazama Arsenal kupitia luninga.

Staa huyo Mjerumani, anayelipwa Pauni 350,000 kwa wiki, amewekwa kando kwenye kikosi cha Arsenal kinachocheza Europa League na Ligi Kuu England.

Ozil, 32, aliandika kwenye mtandao wa kijamii kuhusu klabu hiyo kushindwa kuonyesha uthamini juu yake. Lakini, jambo hilo halikumfanya ashindwe kuendelea kuisapoti timu yake baada ya kutuma ujumbe kwenye Twitter kwamba aliitazama Arsenal ikimenyana na Rapid Vienna kupitia televisheni kwa kuwa hakuwa na kazi nyingine ya kufanya.

Baada ya kusema hivyo, mwongozaji wa kipindi cha BT Sport, Jake Humphrey alimjibu na kumwambia nafasi yake ipo studio.

Ozil aliandika hivi kwenye Twitter: “Kama siwezi kuisapoti timu yangu uwanjani, nitaisapoti kwa kuitazama kwenye televisheni.” Baadaye Ozil aliwataka mashabiki wa Arsenal kutoa utabiri wao wa matokeo kwenye mchezo huo. Humphrey alipoona posti ya Ozil alijibu kwa haraka sana: “Ungana nasi studio Alhamisi ijayo.”

Kisha aliongeza: “Mesut, huu ni mwaliko wa wazi - kama Alhamisi ijayo utataka kuja kuungana nasi, ofa ni hiyo.”

Advertisement

Ozil - ambaye anaweza kwenda Marekani bado hajajibu kitu kuhusu mwaliko huo na kwa sababu hana mazoezi yoyote ya kujiandaa na mechi basi haitaonekana kuwa ni ajabu kama atakubaliana na ofa ya Humphrey.

Wakati huo huo, gwiji wa Arsenal, Martin Keown alisema kuondoshwa kwa Ozil kwenye kikosi kunathibitisha wazi kwamba mchezaji huyo hakubaliki tena kwenye kikosi hicho.

 

Advertisement