Ozil aliyesalitiwa Ujerumani mwenye mali zake Uturuki

LONDON, ENGLAND.UNAPOZUNGUMZIA wachezaji ambao wanakunja mpunga mrefu pale Arsenal na EPL kwa ujumla namba moja ni huyu mwamba kutoka Ujerumani, Mesut Ozil ambaye alisaini mkataba mwaka 2018 unaomfanya kupokea Pauni 350,000 kwa wiki, ikiwa moja ya njia ambazo Arsenal ilizitumia ili kumbakisha kwa kuwa timu nyingi zilionesha nia ya kutaka kumsajili.

Kiujumla Ozil ana utajiri unaokadiriwa kufikia Dola 100 milioni, sambamba na kumiliki mali kibao ikiwa pamoja na mijengo, magari na vyanzo vyengine vya mapato.

Anapigaje pesa

Kwanza ni kupitia mshahara wake wa Pauni 350,000 ambao unamfanya kuwa mchezaji wa pili nyuma ya David de Gea kuwa anakunja mpunga mrefu ndani ya Ligi Kuu, England lakini mbali ya hapo anapiga pesa kupitia dili lake la ubalozi wa kampuni ya Adidas ambalo alisaini miezi michache baada kujiunga na Arsenal na dili la miaka saba linaripotiwa kuwa na thamani ya Pauni 25 milioni.

Mwanzoni mwaka 2017 alisaini mkataba na kampuni ya Beats by Dr Dre ambayo ina wadhamini pia mastaa wa Tottenham na PSG, Harry Kane na Neymar. Lakini mbali na huko jamaa anafanya kazi na kampuni ya BigShoe ambayo inatoa misaada kwa watoto wasiojiweza, hapa yeye ni balozi lakini pesa pia anapiga.

Kampuni nyingine ambayo alikuwa anayofanya nayo kazi ni watengenezaji wa magari ya Mercedes-Benz, lakini ilijitoa baada ya mwamba huyo kuamua kustaafu soka kwa timu ya Taifa kutokana na maneno yaliyoibuka baada ya kuonekana amepiga picha na rais wa Uturuki.

mijengo

Jamaa amewekeza sana, ana mjengo wenye thamani ya Pauni 10 milioni, huko Kaskazini mwa Jiji la London, pia mali zake nyingi zinaripotiwa kuwa Uturuki mahali ambapo anatarajia kuishi ikiwa atastaafu soka. Huko ana mijengo zaidi ya miwili ambayo kwa ujumla ina thamani ya Pauni 8 milioni, sambamba na Hotel alizojenga huko na tayari zimenza kufanya kazi.

Magari

Ana magari zaidi ya matano ambayo ni ya thamani kubwa, ndinga ya kwanza ni aina ya G63 AMG yenye thamani ya Pauni 143, 305 ambayo ni sawa na milioni 423 za Kitanzania pia ana Ferrari 458 kutoka Italia yenye thamani ya Pauni 200,000 ambayo ni sawa na milioni 590 za kibongo, lakini jamaa ana ndinga nyingine kama Audi SUV, SLS AMG, RS5 na Porsche Panamera Turbo ni miongoni mwa sehemu ambazo amewekeza sana.

Msaada wake

katika jamiii

Mwaka 2019 alisaidia watoto 1000 kutoka Uturuki kufanyiwa Upasuaji, sambamba na misaada mbali mbali anayotoa kwa watu wasiojiweza kuna wakati alitoa zaidi ya Euro 300,000 kwa ajili ya kusaidia watoto wasiojiweza huko Brazil. Pia ni mdau mkubwa wa kusaidia watoto yatima kwenye vituo mbalimbali wanavyolelewa.

Kwenye mitandao ya kijamii

Kwenye mtandao wa Instagram ana wafuasi milioni 22, Twitter milioni 25 na Facebook ni milioni 35, huku pia anapiga pesa kwa kufanya matangazo ya kampuni mbalimbali.