Onyango kairudia KO ileile ya Kagere

Sunday October 11 2020
onyango pic

HAKUNA watu wajuaji kama mashabiki wa soka nchini. Wengi wao hujifanya wanajua kila kitu. Wao ndio huwa nji wajuzi kuliko makocha wa timu zao. Ndio maana mara nyingi huwa wanawakosoa na hata kuwatupia maneno ya kejeli viwanjani. Utabisha nini wakati mara kadhaa wamekuwa wakiwatusi ama kuwazomea wakitaka wafanya mabadiliko ya wachezaji kama kwamba wao ndio makocha.

Wakati mwingine hujifanya wao ni waamuzi na wanaojua vyema sheria za soka kuliko hata waamuzi waliozisomea na kuzifanyia kazi kwa muda mrefu viwanjani.

Pia wakati mwingine huwa ni zaidi ya Messi na Ronaldo ndio maana wamekuwa wakiwasakama wachezaji viwanjani wanapokosea kwa bahati mbaya. Mchezaji anapokosa bao huwa wanaeleza alitakiwa kufanya nini ili afunge. Yaani ni wakosoaji wakubwa. Wakati mwingine hujigeuza kuwa watabiri.

Huwa hawana subira wala akiba ya maneno hasa wale wanaoshabikia klabu za Simba na Yanga.

Mashabiki wa klabu hizi ukiwafuatilia namna wanavyowachambua na kuwakosoa kama sio kuwakejeli wachezaji wa timu zao ama wala wa upinzani, ndio utajua namaanisha nini.

Mara nyingi wamekuwa wakiwakejeli sana wachezaji wa kigeni kila wanaposajiliwa na klabu zao. Hata hivyo kwa bahati mbaya mara nyingine wamekuwa wakichemesha na kupigwa KO za aibu na nyota hao.

Advertisement

Unakumbuka usajili wa mara ya mwisho wa Emmanuel Okwi na namna winga huyo Mganda alivyokuwa akikejeliwa na kile alichokifanya uwanjani kabla ya kutimka zake Misri? Unakumbuka usajili wa Meddie Kagere ndani ya Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya misimu mitatu iliyopita? Kagere kma ilivyo kwa Okwi aliitwa mzee. Yeye na Okwi walitajwa kama Wahenga. Waliitwa kwa majina yote ya kejeli, lakini walichokifanya uwanjani, kelele zote dhidi yao ziliyeyuka kama siagi inavyoyeyuka juu ya kikaango cha moto.

Utasema nini juu ya Obrey Chirwa? Kuna watu walimkejeli na kusema Yanga ilichemsha kumsajili. Muda mchache baadaye, wale wale waliokuwa wakimzomea na kumkejeli wakaanza kumshangilia. Utasema nini kwa Simon Msuva? Mashabiki wa klabu yake ya Yanga walimkejeli na kumtukuna. Walidai hakustahili kuichezea Yanga. Walidai ni mtu wa ovyo uwanjani, lakini Msuva aliwajibu kwa vitendo uwanjani. Wale wale waliokuwa wakimkejeli, walibadilika na kuanza kumshangilia na wengine kufikia hatua ya kumbeba viroba vya mchele na kumzawadia uwanjani.

Utasema nini kuhusu ujio wa Lamine Moro? Upande wa Simba ulimponda kwa sababu tu alitemwa Msimbazi akionekana beki wa kiwango cha kawaida. Leo ndio kitasa anayeogopwa hata na watu wa Msimbazi wanapowaza pambano la watani. Hata hawa kina Carlinhos, Mukoko Tonombe, Michael Sarpong na Yacouba Songne nao ilikuwa hivyo hivyo. Upande wa pili ulikuwa ukiwakejeli kwamba ni wachezaji wa kawaida sana. Wengine wakahoji inakuwaje mchezaji kutoka Afrika Magharibi ama Angola

kuja kucheza Yanga? Achana na hiyo, vipi kuhusu Gerson Fraga na wenzake kutoka Brazili? Ni nani leo anayeweza kumkejeli tena Fraga? Juzi kati tena kuna watu walimdisi sana Joash Onyango kutoka Kenya.

Hawakuangalia uwezo wake uwanjani wala rekodi yake ya kuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars walioiadabisha Taifa Stars kwenye mechi ya makundi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2019) pale Cairo Misri. Beki wa kati ambaye hajawahi kuachwa benchi kwenye mechi za Gor Mahia sambamba na timu yao ya taifa.

Mashabiki walimkomalia juu ya muonekano wake wa kuwa kidingi. Walikuwa wakimuita babu na kuamini Simba wamechemsha kumsajili. Wengine walienda mbali na kudai Msimbazi safari hii imeamua kutengeneza ukuta wa maveterani.

Waliuangalia umri wa Erasto Nyoni na ule wa Pascal Wawa kisha kumjumuisha na Onyango wakaona msimu huu watateseka sana kwa wapinzani hasa wenye nyota vijana na wenye kasi. Hata hivyo kwa mara nyingine tena Onyango amewaumbua mashabiki waliomkejeli wakati anakuja nchini ni kama ambavyo Kagere alivyowafanyia alipotua kwa mara ya kwanza na kumuita mhenga.

Misimu miwili mfululizo, Kagere amekuwa Mfungaji Bora tena akiweka rekodi ya mabao na kuwa mchezaji wa kwanza kutetea tuzo hiyo, kitu kilichowashinda wenzake kibao wa kigeni na hata wazawa.

Katika mechi tano za Ligi Kuu Bara za Simba msimu huu, Onyango kaanza zote. Ameupasua ukuta wa Wawa na Nyoni. Amewatenganisha Wawa na Kennedy Juma. Kwa sasa yeye ndiye mfalme mpya Msimbazi kwenye safu ya ulinzi hasa beki ya kati.

Onyango ni kama kamrahisishia kazi Kocha Sven Vandenbroeck katika kupanga mabeki wake wa kati kwa maana mkononi ana jina lake, halafu sasa ni maamuzi yake amuanzishe na Wawa ama Kennedy.

Hapo sijagusia mechi za kirafiki ambazo Simba imeshacheza wala ile ya Ngao ya Jamii.

Wale waliokuwa wakiamini Onyango angesugua benchi mbele ya mabeki aliowakuta kikosini kwa sasa wameumbuka. Wale waliomkejeli kuwa ni babu sasa wanampa heshima yake kimyakimya. Onyango ni bonge la beki. Uzoefu wake wa mechi za kimataifa. Umakini wake katika kuwakaba washambuliaji na jinsi anavyookoa mipira kistadi, inaashiria wazi kuwa, Simba imelamba dume. Namna wanavyocheza kwa ushirikiano na Wawa ni wazi Simba ni moja ya timu yenye ngome ngumu pengine kuliko hata Azam.

Kwenye ligi tayari tumeshamuona. Tumeshaona umahiri wake na sasa mashabiki watamsubiri kwenye michuano ya kimataifa. Simba inaiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na itaanza kibarua chake mwezi ujao. Naamini beki huyo na Wawa wataendelea kusimama pamoja ili kuhakikisha chama lao linafika mbali. Ukweli ndivyo ulivyo. Onyango ni aina ya mabeki ambao Simba ilikuwa ikiwahitaji siku nyingi.

Ilishawahi kumpata kupitia Juuko Murshid, lakini beki huyo kutoka Uganda alikuwa na tatizo la nidhamu. Onyango anacheza kwa nidhamu kubwa. Anatulia akili kuliko nguvu. Pia hampi nafasi straika wa timu pinzani kuleta rabsha langoni mwake. Murshid alikuwa mtamu, ila alijaa vurugu. Alikuwa akicheza soka la kizamani la mabeki wa kati kuwa watemi na wasioremba. Ndio maana ilikuwa hamalizi mechi kadhaa bila kupewa kadi. Onyango yupo tofauti. Huenda alisikia kejeli za mashabiki wa upande wa pili bila kujua kwanini aling’olewa Gor Mahia kuja Msimbazi.

Kupitia mechi alizocheza mpaka sasa bila ya shaka majibu yamepatikana, hata kama ni mapema mno.

Ni kama majibu yaliyopatikana kupitia Chris Mugalu kama sio Mukoko au Yacouba ana Carlinhos ndani ya Yanga.

Nini namaanisha? Ni kwamba mashabiki wajifunze sasa. Kama walishindwa kujifunza kwa kejeli walizowapa kina Heritier Makambo, Papy Tshishimbi, David Molinga, Okwi na Kagere, basi wajirekebishe kupitia kwa Onyango na Carlinhos kama sio Mukoko. Vinginevyo wataendelea kupigwa KO kila mara kwa tabia zao za kupenda kujifanya wajuaji wa mambo na wabashiri wa mambo. Yaani mchezaji alifika tu, wanambashiria kuchemsha na kumponda hata hawajakiona akifanyacho uwanjani.

Huu ni udhaifu mkubwa na kudhihirisha wengi wao ni watu wasiojua kitu, ila wanajifanya wajuaji. Ni dalili za wazi wengi wao ni wakurupukaji ndio maana wamekuwa wakipigwa KO za aibu kila mara. Kama wanabisha waliomponda Onyango na hata Kagere kama sio Lamine wajitokeze tena kuendeleza zile kejeli za awali.

Advertisement