Onyango aisapraizi Simba SC

SIMBA ilifanya usajili wa nyota saba katika dirisha kubwa la usajili mwaka huu lakini kati yao, beki Joash Onyango ndiye ameonekana kutoa mchango mkubwa kikosini na kufiti moja kwa moja katika mbinu za benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha Sven Vandenbroeck.

Licha ya usajili wa Onyango kuwapa wengi hofu wakihisi angepata wakati mgumu kuingia katika kikosi cha kwanza cha Simba, beki huyo raia wa Kenya mwenye umri wa miaka 27, amekuwa nyota muhimu katika safu ya ulinzi ya timu hiyo mbele ya wachezaji aliowakuta kikosini.

Uwezo wa kudhibiti washambuliaji wa timu pinzani, kupora mipira kwa adui, kuokoa mipira ya hewani na chini, kuchezesha timu, hesabu na makadirio sahihi, kasi pamoja na matumizi mazuri ya akili na nguvu, yamemfanya Onyango awe na namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza Simba.

Sifa hizo zimemfanya Onyango kuwa chaguo la kwanza la Simba katika nafasi ya beki wa kati huku akilazimisha wengine waliobakia Pascal Wawa, Kennedy Wilson, Erasto Nyoni na Ibrahim Ame kuwania nafasi moja iliyobakia.

Lakini haijaishia hapo tu kwani Onyango ndiye ameongoza kitakwimu kwa kuwa mchezaji aliyecheza kwa dakika nyingi zaidi kwenye mechi za mashindano kati ya nyota saba ambao Simba imewaongeza kikosini msimu huu huku akiwaacha mbali wengine.

Onyango aliyesajiliwa kutokea Gor Mahia ya Kenya, ameitumikia Simba kwa jumla ya dakika 540 katika mechi sita za kimashindano ambazo imechezea, akianzia katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Namungo iliyoibuka na ushindi wa mabao 2-0 jijini Arusha na baada ya hapo akacheza kwa dakika 90 katika kila mechi kwenye michezo mitano iliyofuata ya Ligi Kuu dhidi ya Ihefu, Mtibwa Sugar, Biashara United, Gwambina na JKT Tanzania.

Katika kundi la wachezaji saba wapya ambao wamesajiliwa na Simba msimu huu, anayemfuatia Onyango ni Bernard Morrison ambaye kacheza kwa dakika 286 katika mechi sita za mashindano ambazo ameichezea Simba hadi sasa.

Baada ya Morrison, mchezaji anayefuatia ni Walter Bwalya ambaye ameichezea Simba kwa dakika 242 huku Chris Mugalu akiwa ameichezea timu hiyo kwa dakika 119 tu kwenye mechi tatu na anayeshika nafasi ya tano ni David Kameta aliyecheza kwa muda wa jumla wa dakika 11 tu.

Beki aliyesajiliwa kutoka Coastal Union, Ibrahim Ame na mshambuliaji Charles Ilanfya, wao ndio wamekuwa na bahati mbaya zaidi katika kikosi cha Simba hadi sasa kwani hawajacheza mechi yoyote ya kimashindano tangu wajiunge na timu hiyo kuanzia ile ya Ngao ya Jamii hadi zile tano za Ligi Kuu.

Onyango hajaishia tu kuwakimbiza wenzake saba ambao wamejiunga na Simba kwa wakati mmoja bali pia ameingia katika orodha ya wachezaji wanne waliotumikia Simba kwa dakika nyingi msimu huu.

Wengine ni kipa Aishi Manula, mabeki Mohamed Hussein na Shomari Kapombe.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu ambaye pia kitaaluma ni kocha alisema kinachombeba Onyango kucheza michezo mingi ni mabeki wakongwe, Erasto Nyoni na Pascal Wawa kuanza msimu wakiwa majeruhi.

Rweyemamu alisema hata hivyo uzoefu wa Onyango, kupevuka na ufahamu wake vilimbeba beki huyo na kuwa mtu muhimu katika ukuta wao akifanikiwa kuwa bora kuliko wengine.

“Kuna changamoto lazima tuziangalie kwenye hili la Onyango,wakati tunaanza msimu mtakumbuka Nyoni alikuwa mgonjwa pamoja aliyechelewa kujiunga na timu lakini pili kuna suala la uzoefu,kupevuka kwake na ufahamu.

“Kwenye changamoto hizo unakuja kukuta tulibaki na Kennedy (Juma) pekee ambaye sasa ukimuongeza na Ame (Ibrahim) tunakuwa na mabeki watatu pekee kwahiyo kwa akili ya kawaida tulitaraji kuona, Kennedy pekee ndio ataanza kuwa juu.

“Ame hatuwezi kumlinganisha na Kennedy kwa kuangalia uzoefu, ufahamu na upevukaji ndio maana tuliamua kuanza kuwatumia Kennedy na Onyango lakini sasa anafanya vizuri.”