Ole na siku 4 kuokoa ajira

 LONDON ENGLAND. GARY Neville kawa mkali kuhusu Manchester United na ishu yao ya usajili kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi. Mwingereza huyo ameiambia klabu yake hiyo ya zamani kwamba inafanya biashara ya usajili kizembe.

Kocha Ole Gunnar Solskjaer anataka kuongeza mastaa wapya kabla ya dirisha kufungwa huku akiwa na matumaini ya kwamba atamnasa Jadon Sancho kutoka Borussia Dortmund.

Na Neville amewaambia Man United hakuna ujanja mwingine zaidi ya kusajili tu kabla ya dirisha kufungwa ili kujenga kikosi kitakachokuwa na nguvu kwenye ushindani wa mataji dhidi ya wapinzani wao kwenye ligi.

Wakati dirisha la usajili katika majira haya ya kiangazi likitarajiwa kufungwa Jumatatu ijayo, Man United imeripotiwa kwamba ofa yao ya Pauni 91 milioni imegomewa na Dortmund juu ya mchezaji Sancho. Wajerumani hao wanang’ang’ania Pauni 108 milioni na hivyo, Man United wamerudi kujipanga upya.

Ukiweka kando dili la Sancho, mastaa wengine ambao Man United inapambana kunasa huduma yake kabla ya dirisha hili kufungwa ni mkali wa Barcelona, Ousmane Dembele - ambaye atanaswa kwa mkopo wa msimu mzima.

Man United inapiga hesabu za kumnasa beki wa kushoto wa FC Porto, Alex Telles - lakini Neville anawaambia Man United wasiache pia kusajili beki wa kati, kwa sababu anahitajika sana.

“Huu ni usajili ambao ni rahisi sana kupata mchezaji kwenye historia ya Ligi Kuu England, lakini Man United hakuna inachokifanya,” alisema Neville na kuongeza. “Wanapaswa kumpatia Ole beki wa kati, beki wa kushoto na mshambuliajia kabla ya dirisha kufungwa. Mbona wengine wanasajili kirahisi tu, kwanini Man United!”

Mashabiki wanadai itakachokifanya Man United kwa sasa ni kufanya usajili wa kupaniki. Hadi sasa United imemsajili Donny van de Beek kwa Pauni 39 milioni.