Ole amtaka Rashford afunge mabao 20

Wednesday August 14 2019

 

MANCHESTER, ENGLAND. OLE Gunnar Solskjaer ameripotiwa kumpa straika wake Marcus Rashford kazi ya kufunga mabao 20 kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Rashford ataingia kwenye msimu huu akiwa straika namba moja wa Manchester United, huku akionyesha makali mapema baada ya kufunga mara mbili katika mchezo wa kwanza wa ligi hiyo dhidi ya Chelsea uwanjani Old Trafford Jumapili iliyopita.

Ole amempa mtihani mzito mshambuliaji huyo, ambaye kwenye maisha yake ya soka huko Man United tangu aanza kuchezea kikosi cha kwanza hajawahi kufunga mabao kuzidi 14 katika michuano yote ndani ya mwaka.

Lakini, sasa kocha Solskjaer alizungumza na mshambuliaji huyo wiki iliyopita na kumtaka afunge zaidi ya mabao 20 msimu huu. Kocha huyo alimnoa vyema kabisa mshambuliaji wake kwenye majira ya kiangazi ili kuhakikisha anakuwa mfungaji bora wa Man United kwa msimu huu.

Taarifa ya kutoka Old Trafford ilifichua: “Ole aliketi kitako na Marcus wiki iliyopita. Yalikuwa mazungumzo mazuri. Walizungumza kama kwa nusu saa hivi, akimwambia vitu ambavyo anataka avifanye kwenye msimu huu.

“Ole alimfundisha namna ya kuingia ndani ya boksi zaidi na kucheza karibu na goli. Mwanzoni ilikuwa ikitegemewa sana mipira ya ju, lakini sasa matarajio makubwa yatakuwa kwenye mipira ya chini inayopigwa katikati ya mabeki wa kati wa timu pinzani.”

Advertisement

Rashford anafahamu wazi kwamba ni jukumu lake la kuibeba Man United msimu huu baada ya timu hiyo kumpiga bei aliyekuwa straika wao namna moja, Romelu Lukaku na hakuna mbadala wake aliyesajiliwa. Washambuliaji wengine wa Man United ndani ya msimu huu ni Anthony Martial, Alexis Sanchez na Mason Greenwood.

Advertisement