Oktay ajishasha kisa Gor Mahia

Tuesday January 28 2020

 

By Thomas Matiko

KOCHA aliyewaacha Gor Mahia kwa mataa Hassan Oktay kadai klabu hiyo imemfungulia milango ya kheri na kumfanya kuitiwa ofa za nguvu tangu alipowakimbia.

Oktay aliyeigura Gor miezi mitano iliyopita kasema klabu hiyo ilimfanya kuwa maarufu sana jambo ambalo limesababisha klabu kadhaa kuulizia huduma yake.

Mkufunzi huyo Mturuki aliteuliwa kuifunza Gor Desemba 2018 na kuwaongoza kutetea taji lao la ligi kuu.

Agosti 2019 aliomba likizo ya siku tano kwenda kumcheki mama yake aliyekuwa akiugua na siku hizo za likizo alizokuwa ameomba zilipokaribia kuisha, aliandika barua ya kujiuzulu wadhifa wake. Sababu ya kuondoka ni kucheleweshewa mshahara lakini kubwa zaidi, zipo klabu zilizokuwa zikimuulizia huduma yake.

Akifunguka na jarida la kimichezo People’s Sport, Oktay anasema kwa sasa kapokea ofa kama zote kwa sababu kawa maarufu na jina lake ni kubwa kwenye ulimwengu wa ukocha hapa Afrika.

“Mbeleni sikuwa nikijulikana ila baada ya kuwafunza Gor, sasa hivi mimi ni jina kubwa. Sijui kama Wakenya wanaelewa ni jinsi gani Gor ni klabu kubwa huku nje. Gor wamenifungulia milango ya kheri, nimepokea ofa tatu nzuri. Nkana FC wa Zambia, Rayon Sports wa Rwanda na klabu nyingine kutoka Botswana zote zimeniulizia. Kwa sasa natathimini ofa hizo kabla ya kufanya uamuzi,” Oktay aliyeteuliwa kurithi mikoba ya Mwingereza Dylan Kerr kajishasha.

Advertisement

Kabla hajajiunga na Gor, Oktay alikuwa naibu kocha wa klabu ya Braintree Town FC inayoshiriki divisheni ya tano kule Uingereza.

Advertisement