Nyota saba Humburg FC waisaka safari ya Brazil

Muktasari:

Kwa niaba ya wachezaji wenzake, Nahodha Abdulrahim Faiz ameliambia Mwanaspoti watapigana na kucheza soka la hali ya juu ili kushinda shindano hilo la kitaifa kwa sababu wana hamu ya kwenda Brazil kumshuhudia Neymar live.

KONGOWEA. HAMBURG FC inatarajia kuondoka Mombasa hapo kesho Ijumaa kuelekea Nairobi ambapo itashiriki kwenye mashindano ya ngazi ya kitaifa ya Neymar Junior Five-a-side ambayo mshindi wake atafuzu kufanya ziaya ya kwenda nchini Brazil.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abubakar Omar Batistuta amesema wachezaji wake saba watakoshiriki kwenye dimba hilo la mashindano ya soka ya wachezaji watano kila upande yatakayofanyika jijini Nairobi kuanzia kesho usiku hadi Jumapili, wamepania kupata ushindi.

“Ingawa tuko mwezi wa mfungo wa Ramadhan, tumejiandaa vya kutosha wanasoka wangu wamepania kuhakikisha wanashinda kwani wana hamu ya kufuzu kwenda Brazil kukutana na Neymar, mmoja wa wachezaji wenye kutambulika duniani,” akasema Batistuta.

Kwa niaba ya wachezaji wenzake, Nahodha Abdulrahim Faiz ameliambia Mwanaspoti watapigana na kucheza soka la hali ya juu ili kushinda shindano hilo la kitaifa kwa sababu wana hamu ya kwenda Brazil kumshuhudia Neymar live.

“Pia tutapata fursa ya kuvutia maskauti watakaokuwako ambao wanaweza kutusajili baadhi yetu tucheze soka la kulipwa huko Amerika Kusini ama sehemu nyingine za Bara la Ulaya,” akasema Faiz.

Wachezaji watakaowakilisha Hamburg huko Nairobi ni Faiz (Nahodha), Said Miraj, Walid Ahmed, Maulidi Ali, Mbarak Abdalla, Ahmed Abdul na Omar Ahmed. Maofisa ni Batistuta (Kocha Mkuu), Abdalla Harun (Naibu Kocha), Abubakar Ahmadala (Meneja), Stephen Mwanzia (Naibu Meneja) na Ahmed Salim (Mfadhili).