Nyota Taifa Stars: Rwanda kipimo tosha cha kuwapiga Sudan

Muktasari:

Tanzania kujipima ubavu na Rwanda kunawaaminisha nyota wa kikosi hicho kwamba wamepata kipimo sahihi cha kujiandaa mechi na Sudan ya kufuzu fainali za CHAN.

Dar es Salaam. Wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, beki Boniface Maganga na kipa Metacha Mnata wamesema mechi ya kirafiki dhidi ya Rwanda ni kipimo sahihi kwao kujiandaa na Sudan.

Taifa Stars imelazimisha suluhu na Rwanda jana Jumatatu katika mchezo wa kirafiki wa kujianda na mechi yake ya kusaka kufuzu kwa CHAN2020 dhidi ya Sudan itakayochezwa Ijumaa wiki hii.

Maganga alisema Rwanda ni timu yenye ushindani, hivyo anaamini wamejengeka kiufundi na kujipa matumaini makubwa ya kushinda dhidi ya Sudan licha ya kwamba walifungwa mechi nyumbani kwa bao 1-0.

"Naamini kucheza na Rwanda ni kipimo chetu sahihi, kikubwa Watanzania watuunge mkono ili nguvu ya pamoja itumike kuwafunga Sudan kwao,"

"Kiufundi tupo vizuri, kocha anaendelea kutujengea mbinu za kujiamini bila shaka tutazifanyia kazi uwanjani kupata matokeo,"alisema Maganga.

Naye kipa Mnata alisema wanajua wazi watakumbana na changamoto ya ushinda katika mchezo wao na Sudan, lakini wanajipa matumaini ya kurejea na ushindi.

"Ushindani utakuwa mkali kwenye mchezo huo, ila tuna imani kupata ushindi, mechi ya kirafiki na Rwanda ambayo tumecheza tunaamini imetuongezea kujiamini zaidi,"alisema Mnata.