Nyota 13 wazipangua Simba, Yanga

Tuesday August 13 2019

 

By Khatimu Naheka

SIMBA na Yanga zimeshacheza dakika 90 kila moja katika Ligi ya Mabingwa msimu huu, lakini katika vikosi vyao majina 13 yakapindua meza yakichomoza katika vikosi vya kwanza.

Tuanze na Simba ambayo wikiendi iliyopita ilikuwa pale Msumbiji ikianza na suluhu na wenyeji, UD Songo ya huko. Katika kikosi chake kilichoanza na wachezaji 11 katika mechi hiyo kilikuwa na sura nne zilizopindua meza.

Simba ilianza na kipa Benno Kakolanya langoni akichukua nafasi ya Aishi Manula aliyekuwa majeruhi, lakini hatua hiyo inaweza kuwa mwanzo bora kwa kipa huyo mpya aliyetokea Yanga kwa kuanza bila kuruhusu bao.

Msimu uliopita, Simba ilimtumia sana Manula katika mechi zake ambapo hakuna mechi ya ugenini kipa huyo aliyomaliza bila kuruhusu bao na kama Kakolanya akiendelea na uwezo bora huu, basi anaweza kuwa changamoto kwa Manula.

Katika ukuta wa timu hiyo ingizo jipya aliyepindua meza alikuwa Gadiel Michael ambaye alimfanya nahodha wake msaidizi, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kusugua benchi.

Pia, Shomari Kapombe alirejea katika nafasi yake ingawa haonekani kama mtu mpya sana na kama angekuwa sawa kiafya hata msimu uliopita angeanza kutokana na kumzidi mambo mengi beki aliyetupiwa virago, Zana Coulibaly.

Advertisement

Katika kiungo, Simba ilikuwa na mtu mwingine raia wa Sudan, Ali Abdulraman Shiboub ambaye anachukua nafasi ya James Kotei aliyeachwa na Wekundu hao huku katika kiungo wa ushambuliaji wakiwa na Mkenya, Francis Kahata aliyeingia kikosi cha kwanza akichukua nafasi ya Mganda Emmanuel Okwi.

Simba ina watu saba pekee ambao wamefanikiwa kutunza nafasi zao katika kikosi hicho ambao ni mabeki Pascal Wawa, Erasto Nyoni huku viungo wakiwa Jonas Mkude na Clatous Chama wakati safu ya ushambuliaji ikiwa na Meddie Kagere na nahodha wao John Bocco. Wakati hali ikiwa hivyo Simba, pale Yanga kuna majina matatu pekee yaliyofanikiwa kubakiza nafasi zao katika kikosi cha wachezaji 11.

Yanga ndio timu iliyokuwa na mabadiliko makubwa kutokana na udhaifu wa kikosi chao cha msimu uliopita ambapo sasa ina watu wapya wanane walioingia kikosi cha kwanza.

Katika safu ya ulinzi anzia kwenye nafasi ya golikipa, Yanga ina mtu mpya, Metacha Mnata ingawa huenda nafasi yake ikachukuliwa na mwingine mpya, Mkenya Farouk Shikhalo ambaye kama si kukosa vibali basi angesimama golini katika mchezo dhidi ya Township Rollers.

Beki wa Yanga, Paul Godfrey ndiye pekee aliyefanikiwa kubakiza nafasi yake baada ya timu hiyo kuanza na watu wapya Lamine Moro, Ally Mtoni na Mharami Issa.

Hata hivyo, ukuta huo unaweza kubomoka kama mkongwe Kelvin Yondani atarejea kazini ambapo atawafanya Lamine au Sonso mmoja kusogea nafasi nyingine au hata kusubiri benchi.

Safu ya kiungo, nahodha wa timu hiyo, Papy Tshishimbi amefanikiwa kuilinda nafasi yake huku pia Mohamed Issa ‘Banka’ licha ya kutoanza mara kwa mara msimu uliopita amefanikiwa kuingia kikosi cha kwanza.

Safu ya ushambuliaji nzima imeingiza watu wapya ambapo viungo wa pembeni Mapinduzi Balama, Patrick Sibomana na Sadney Urikhob wamechukua nafasi.

Wasikie wachambuzi

Akichambua hatua hiyo ya mabadiliko, mchambuzi wa soka Ally Mayay ameliambia Mwanaspoti kuwa mabadiliko yaliyofanywa na Yanga yanatokana na kikosi chao cha msimu uliopita kuwa katika hali mbaya, huku Simba ikiendeleza maboresho ya kikosi chake bora.

“Simba imekuwa kama na mwendelezo wa kikosi bora pamoja na kuondoka kwa mtu kama Okwi, lakini timu yao imeendelea kuimarika,” alisema Mayay.

“Ukiangalia Yanga walihitaji sana mabadiliko ya kikosi chao, msimu uliopita asilimia 70 ya wachezaji wao hawakuwa na ubora wa kuichezea timu hiyo hata Tshishimbi hakuwa yule ambaye wa wakati anafika ingawa sasa anaonekana amebadilika.

“Shida kubwa msimu huu Ligi ya Mabingwa Afrika imeanza kabla ya ligi haijaanza, unajua mechi za ligi zilikuwa na faida yake kwa kuziandaa timu kiushindani na kuzimarisha tofauti na kinachoendelea sasa.

“Simba bado inaendelea kufurahia upana wa kikosi chake, hii itaisaidia, kocha atakuwa na mzunguko wa wachezaji katika mechi mbalimbali, msimu ujao mechi zitakuwa nyingi na sioni kama kutakuwa na viporo tena kwa timu waliyonayo, itawanufaisha.”

Naye Kennedy Mwaisabula alisema mabadiliko makubwa ya timu hizo hasa Simba ni mwendelezo wa hulka ya kupenda kufanya usajili mkubwa mwisho wa msimu.

Kocha huyo wa zamani wa Yanga, alisema timu hiyo inahitaji mabadiliko makubwa katika kikosi chake tofauti na Simba ambayo katika mabadiliko iliwaacha wachezaji ambao bado walikuwa na uwezo wa kuitumikia timu yao.

“Timu zote mbili mwisho wa msimu huwa zinawaacha wachezaji wao hata kama bado wana uwezo, hii ni hulka yetu na imeanza miaka ya 2000 kuja mbele. Kuna wachezaji wameachwa wakiwa bado wana nafasi ya kuendelea kuwepo, mfano Kotei wa Simba alikuwa bado ana uwezo,” alisema Mwaisabula.

“Yanga ilihitaji mabadiliko makubwa zaidi kutokana na aina ya timu iliyokuwa nayo msimu uliopita, haikuwa na ubora mkubwa wa kushindana.

“Mabadiliko haya kwa timu zote yanaweza kuwa na matokeo chanya, mfano kama Yanga ya msimu huu ni tofauti na ile ya mwaka jana, angalau sasa ina watu ambao unaona wanaweza kuwa na ushindani. Simba naona itaimarika, ni kama imeongezea nguvu timu yao kwa baadhi ya nafasi, ingawa kuna maeneo ingeweza kuyaacha na kuendelea na watu walewale.

“Angalia Manchester United imerudi na watu wengine wa msimu uliopita, waliona bado wana uwezo.”

Advertisement