Nyie Simba, Yanga sikieni hii!

Tuesday September 15 2020

 

By OLIPA ASSA

KIPA wa Mtibwa Sugar, Said Mohamed ‘Nduda’ amesema sare zilizopata Simba na Yanga kwenye mechi tofauti, anaamini zimetoa uhalisia wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), itakavyokuwa msimu huu.

Nduda alisema kwa namna timu hizo zilivyosajili na jinsi mashabiki wao wanavyotamba mtaani, ingekuwa ndio vitendo uwanjani, basi timu nyingine zisingekuwa zinaingiza wachezaji uwanjani.

Alifafanua kwamba ukubwa wa majina ya mastaa wao unawasahaulisha ushindani halisi uliopo kwenye ligi hiyo, jambo ambalo anaamini sare ilizopata Simba dhidi yao na Yanga kwa Prisons, zimewapa picha kamili ya nini watakutana nacho.

“Usajili wa Simba na Yanga jinsi ambavyo unakuzwa, unakuwa unawapa matumaini makubwa mashabiki wao kujua kila mechi kwao inakuwa rahisi. Naamini kabisa matokeo yao ya sare yatawafumbua macho kwamba ligi ni ushindani na sio rahisi,” alisema na kuongeza kuwa:

“Mfano kuna wachezaji wapya ndani ya kikosi cha Yanga ambao walikuwa wanatajwa zaidi kuliko hata wale waliokuwa na timu ambao ndio wazoefu.

“Kitendo cha kutoka sare na Prisons kiliwashitua mashabiki kujua uhalisia wa ligi ulivyo, vivyo hivyo kwa Simba, nao watajua kila timu inayoshiriki Ligi Kuu ipo kwa ajili ya kushindana.”

Advertisement

Naye winga wa timu hiyo, Haruna Chanongo akichangia hoja ya Nduda, alisema kwamba kwa wachezaji wa kigeni angalau Clatous Chama wa Simba tayari ameonyesha ana kitu kwa ajili ya wazawa kujifunza kwake.

“Tunawasubiri hao wengine tuone watafanya nini baada ya majina yao kuwa makubwa kabla ya kazi, tofauti na Chama ambaye tayari ameonyesha ana kitu gani ambacho hata mzawa anajifunza kutoka kwake,” alisema Chanongo na kuongeza kuwa.

“Hata wakati tunajiandaa kucheza na Simba, mchezaji kama Chama alikuwa anatupasua kichwa ni namna gani tunaweza tukamdhibiti, kuna wakati hata mashabiki wanaweza wasione tunafanya nini lakini sisi tunaocheza tunajua moto wake.”

 

 

Advertisement