Niyonzima aibua hofu Yanga SC, Morrison kuwavaa Kagera

Muktasari:

Mapinduzi Balama aliumia kifundo cha mguu akiwa mazoezini, huku Pappy Tshishimbi akisumbuliwa na maumivu ya nyama za paja na Haruna Niyonzima akiumia katika mchezo dhidi ya Biashara Unite, juzi.

Dar es Salaam. Kocha Luc Eymael wa Yanga hofu imekuwa kubwa baada ya nyota wake kupata majeraha mfululizo hivi karibuni huku wakiwa na michezo miwili migumu mbele yao.

Mapinduzi Balama aliumia kifundo cha mguu akiwa mazoezini, huku Pappy Tshishimbi akisumbuliwa na maumivu ya nyama za paja na Haruna Niyonzima akiumia katika mchezo dhidi ya Biashara Unite, juzi.

Yanga ina kibarua kigumu dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo utakaopigwa kesho kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, huku Jumapili ikiwa na kibarua kingine cha nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Simba mchezo utakaopigwa katika Uwanja wa Taifa.

Akizungumza na Mwananchi, Eymael alisema kuumia kwa wachezaji wake nyota ni pigo, lakini hana jinsi baada ya hali hiyo kutokea. “Inaumiza lakini hakuna jinsi zaidi ya kukabiliana na hili ambalo linaendelea, Tshishimbi mgonjwa, Balama mgonjwa na Niyonzima naye hivyohivyo,” alisema.

“Kukosekana kwa Niyonzima itakuwa pigo kutokana na uwezo wake uwanjani na pia ni mchezaji nyota katika kikosi cha kwanza na hilo linajulikana, lakini ngoja tuone inakuwaje katika upande wa afya yake.”

Kocha huyo aliongeza kuwa anasubiri daktari na mnyoosha misuli wa timu wamkabidhi ripoti ili aione itasemaje kabla ya mchezo wao dhidi ya Simba.

“Sijajua watakuwa nje kwa muda gani mpaka muda huu, nasubiri kupata ripoti ya daktari pamoja na mwenzake tuone kwamba watakuwa nje kwa muda gani, lakini nadhani watauwahi mchezo dhidi ya Simba,” alisema.

Morrison atua Kagera

Wakati Niyonzima akipata majeraha, Kocha Eymael akili yake imemgeukia winga mshambuliaji Bernard Morrison kwa ajili ya kuongeza nguvu kikosini.

Eymael alisema mchezaji huyo ambaye aliachwa Dar es Salaam tayari yupo Bukoba kwa ajili ya mchezo.

Uwepo wa Morrison utaongeza nguvu kikosini licha ya kwamba amekuwa kwenye mgogoro na uongozi wa klabu hiyo juu ya suala la mkataba anaodaiwa kuongia na timu wa miaka miwili.

Aitaka Simba uwanjani

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Morrison alisema yuko tayari kwa mechi zote ikiwamo dhidi ya Simba.

“Natamani tena kuifunga Simba, sio mechi hiyo tu, hata nyingine zilizosalia,” alisema na kuongeza kuwa anaamini Yanga itafanya vizuri na kutwaa ubingwa wa FA ili kukata tiketi ya kuiwakilisha nchi kimataifa.

Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema mchezaji huyo tayari amejiunga na timu jana mchana.

“Tumeingia naye Bukoba muda si mrefu (jana saa 7 mchana), atafanya mazoezi ya pamoja na wenzake na ishu ya kucheza au

kutocheza kocha ndiye ataamua,” alisema.

 

Kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’ alisema kitendo cha Morrison kurejeshwa moja kwa moja sio jambo la kushangza kwani ni mchezaji halali wa Yanga.
“Morrison bado ana mkataba na Yanga, kwa hiyo ni mchezaji wa halali pale, uongozi kuamua kumpeleka si jambo baya kabisa kwa sababu anaenda kazini kwake na Yanga ndio mabosi wake, nawapongeza viongozi wa Yanga kwa kufanya hivyo kuziba pengo la Niyonzima kwa haraka,” alisema.

Akizungumzia vuguvuvu linaloendelea kati ya Yanga na mchezaji hali lililomfanya Morrison kuwa na ‘ingia toka ‘katika kikosi cha Yanga hivi karibuni, Mwaisabula alisema Yanga ni kama baba kwa mchezaji huyo hivyo inabidi ijue namna ya kumlea mtoto.
“Sawa, Morrison labda ana tabia fulani za utata, lakini hapa nyumbani tuliwahi kuwa na Juma Nyosso na Haruna Moshi ‘Boban’ lakini wote kwenye mechi walikuwa wanafanya vizuri na kila mmoja anajua, hivyo Morrison avumiliwe.”

Nahodha wa zamani wa Yanga ambaye pia ni mchambuzi wa soka, Ally Mayai alisema kitendo cha mchezaji huyo kurejeshwa sio cha kushangaza kwa sababu ni mchezaji halali wa Yanga.

“Unajua huyu suala lake lilienda mpaka kwenye Shirikisho (TFF) na likaamuliwa vizuri kwa hiyo sio kitu cha kushangaza, Fifa (Shirikisho la Soka duniani) wanataka mchezaji aliye na mkataba na timu aweze kucheza, kwa hiyo kucheza ni moja ya kazi yake,” alisema. (Nyongeza na Imani Makongoro)