MTU WA PWANI : Ninja anatupooza machungu ya Yondani, Aggrey

Saturday July 6 2019

 

By Charles Abel

MUDA mfupi baada ya Taifa Stars kuondolewa kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ alikamilisha uhamisho wa kujiunga na MFK Vyskov ya Jamhuri ya Czech.

Ninja aliyejiunga kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga, anakuwa Mtanzania wa pili kusajiliwa na timu hiyo akifuata nyayo za nyota wa timu ya taifa ya vijana, Ally Nganzi ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo klabu ya Forward Madison inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu Marekani.

Habari nzuri zaidi, mara baada ya Ninja kukamilisha uhamisho huo baada ya kusaini mkataba wa miaka minne, atapelekwa kwa mkopo klabu ya LA Galaxy inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani.

Kwa Ninja huu unaweza kuwa uamuzi bora zaidi kwa maendeleo yake kwa maana ya kuzidi kuimarisha kiwango chake kwani anakwenda kuingia katika mfumo na maisha ya kisasa zaidi kisoka, pia ni faida kwake kwa kuboresha kipato chake kwa maana anakwenda kupata fedha nyingi zaidi ya zile ambazo alikuwa akipata nchini.

Lakini kwa upande mwingine uhamisho wa Ninja unaweza kuwa ni ukombozi kwa Taifa Stars kwani umekuja kipindi ambacho inaelekea kupata pengo la kuondokewa na wachezaji watatu muhimu safu yake ya ulinzi ambao ni mabeki wawili wa kati Kelvin Yondani na Aggrey Morris sambamba na kiungo kiraka anayeweza kucheza pia nafasi hiyo, Erasto Nyoni.

Katika umri wa miaka 34 ambao Yondani anao na ule wa Morris wa miaka 35 ni wazi maisha ya nyota hao wawili kwenye kikosi cha Stars sio marefu baada ya kuitumikia timu hiyo kwa zaidi ya miaka 10.

Advertisement

Inasemekana kuwa baada ya Stars kuondolewa kwenye fainali za AFCON wawili hao pamoja na Erasto Nyoni mwenye umri wa miaka 31, wako mbiono kung’atuka kuichezea timu hiyo ili kupisha damu changa kikosini baada ya wao kutimiza ndoto za kuifikisha nchi ya ahadi.

Lakini kwa bahati mbaya, ukitazama kundi kubwa la nyota waliobakia hapa nchini ambao wanacheza nafasi zao, hakuna ambaye anaonekana ana sifa ama vigezo vinavyoshabihiana na watatu hao.

Matumizi makubwa ya akili na yale ya wastani ya nguvu pindi wanapokabiliana na washambuliaji wa timu pinzani, utulivu wa hali ya juu walionao pamoja na uwezo wa kuwapanga mabeki wenzao na pia kushiriki katika mashambulizi, ni sifa ambazo zimetengeneza utofauti mkubwa baina ya Nyoni, Morris, Yondani na mabeki wengine wa kati hapa Tanzania.

Daraja hili la ubora ambalo linawatofautisha watatu hao na mabeki wengine, hapana shaka ndilo linalowaumiza kichwa wadau wa soka kutafakari ni watu gani sahihi wataweza kuvaa viatu vyao mara baada ya wao kuipa mkono wa kwaheri Stars.

Ukiangalia kundi kubwa la mabeki wa kati ambao huu unapaswa kuwa wakati wao kucheza Stars, wengi hawana utulivu na wamekuwa wakifanya makosa ya mara kwa mara ambayo yanaleta shaka kuwapa nafasi kikosini.

Ingawa wana maumbo mazuri ya kucheza nafasi hiyo, wanakosa baadhi ya vitu muhimu vya kimsingi vya kuwawezesha kukaribia daraja la wakongwe hao watatu ambao wanaelekea kutandika daruga kwenye timu hiyo.

Kwa Ninja kwenda kucheza Marekani, maana yake atakutana na makocha bora zaidi ambao watamtengeneza na kumfanya awe beki aliyekamilika na mwenye vigezo vya kiufundi kucheza kwenye nafasi ya beki wa kati.

Akiwa huko maana yake atakutana na wachezaji wa daraja la juu ambao watamuimarisha kiushindani jambo litakalomjengea uzoefu na ubora utakaoisaidia Stars kwa muda mrefu.

Ni wazi kwamba soka la kulipwa nje ya nchi litamtengeneza Ninja wa tofauti na yule aliyezoeleka na litambadili na kumfanya awe mchezaji wa kisasa tofauti na yule aliyeichezea Yanga au Taifa ya Jang’ombe ya Zanzibar.

Wakati umefika sasa kwa mabeki wengine vijana nchini kama vile Bakari Mwamnyeto, David Mwassa, Paul Bukaba, Ismail Gambo na Ally Ally kutazama fursa nje ya nchi na kufuata nyayo za Ninja ili nchi yetu ipate wachezaji bora wa daraja la juu ambao watakuwa na msaada kwa timu yetu ya taifa siku za usoni.

Advertisement