Ni wa hapahapa wameshindwa kuvumilia kucheza soka nje

Muktasari:

Makala haya yanakuletea baadhi ya wachezaji wa Tanzania ambao walipata nafasi ya kucheza soka Ulaya na ndani ya Afrika katika nchi ambazo zimeendelea kisoka, lakini walishindwa kuonyesha uvumilivu na kurudi nyumbani kucheza soka.

Baadhi ya wapenzi wa soka na ambao si wapenzi wana hamu ya kumuona nahodha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mbwana Samatta akicheza mechi ya kwanza akiwa na timu mpya ya Aston Villa ya England.

Kuna wimbi kubwa la wachezaji hapa nchini ambao kwa nyakati tofauti wamewahi kupata nafasi ya kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, lakini wameshindwa kuwa na mwendelezo mzuri kama ambao ameonyesha Samatta, wakiishia kurudi nchini. Makala haya yanakuletea baadhi ya wachezaji wa Tanzania ambao walipata nafasi ya kucheza soka Ulaya na ndani ya Afrika katika nchi ambazo zimeendelea kisoka, lakini walishindwa kuonyesha uvumilivu na kurudi nyumbani kucheza soka.

SHOMARY KAPOMBE

Beki wa kulia wa Simba - kwanza alipata nafasi ya kwenda kufanya majaribio katika klabu ya FC Twente ya nchini Uholanzi, ambapo ilishindikana kwenda huko na uongozi wa timu yake msimu wa 2013–14 ulimuuza kwenda kucheza nchini Ufaransa katika klabu ya Cannes. Kapombe alicheza Cannes kwa msimu mmoja tu na mwanzoni mwa 2014 alirudi nchini na kusajiliwa na Azam FC ambayo alikaa nayo mpaka 2017 alipokwenda kujiunga na timu yake ya awali, Simba, anayoicheza sasa.

HARUNA MOSHI ‘BOBAN’

Kiungo mtukutu ambaye ana kipaji kikubwa cha soka aliweza kuitumikia Simba kwa mafanikio makubwa kiasi cha kuuzwa nchini Sweden kwenye klabu ya Gefle FC inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo - tena kwa kiasi kikubwa cha pesa.

Ingawa nyota huyo hakudumu sana na timu hiyo baada ya kuvunja mkataba kutokana na madai ya kutopata maslahi mazuri, lakini Simba ndio iliyomtoa hadi kumfikisha kwenye hatua ya kucheza soka la kimataifa, na kwa sasa yupo nchini na anachezea timu ya Singida United.

MRISHO NGASSA

Alipata nafasi ya kufanya majaribio katika nchi mbalimbali za Ulaya, lakini alipata pia ofa za maana katika timu kubwa za soka hapa Afrika, ila zote aliamua kuzipiga chini.

Ngassa alifanya hivyo baada ya kukataa kwenda kucheza katika baadhi ya timu kubwa, lakini 2015-2016 alisajiliwa na timu ya Free State Stars ya Afrika Kusini.

Baada ya hapo alikwenda Fanja ya Oman 2016-17, na baadaye aliamua kurudi kucheza soka la hapa nchini katika timu za Mbeya City, Ndanda na kisha Yanga ambako ndiko yupo mpaka sasa.

SHABAN CHILUNDA

Baada ya kupandishwa katika timu ya wakubwa ya Azam, alicheza katika kiwango kizuri na mwaka 2018-19 alisajiliwa na timu ya Deportivo Tenerife ya Hispania ambao baada ya kumuona ameshindwa kufanya vizuri walimtoa kwa mkopo timu ya Deportivo Izarra ya huko. Baada ya kuona mambo yanashindwa kumuendea vizuri mwaka huohuo (2019), aliamua kurudi kucheza soka hapa nyumbani katika timu yake ya Azam FC, ambako ndiko aliko mpaka wakati huu.

SHIZA KICHUYA

Januari mwaka jana, winga huyu mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania alikamilisha usajili wa kujiunga na klabu ya Pharco inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Misri, lakini baada ya kukamilisha usajili huo alitolewa kwa mkopo katika timu ya Enppi inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo.

Kichuya alikaa katika timu hiyo kwa miezi sita tu na kuwashtua wafuatiliaji wengi wa soka baada ya kuamua kurudi tena nchini katika dirisha dogo la usajili lililopita akisaini mkataba wa kuitumikia timu yake ya zamani, Simba.

DEO MUNISHI ‘DIDA’

Baada ya kumaliza mkataba wa kuitumikia Yanga mwaka 2016, aliondoka nchini na kwenda kucheza soka la kulipwa Afrika Kusini katika klabu ya University of Pretoria, ambapo alicheza si zaidi ya miaka miwili kisha alisajiliwa na Simba kwa mkataba wa mwaka mmoja msimu uliopita na mara baada ya kumalizika aliachwa.

Baada ya Simba kuamuacha msimu huu alikuwa mchezaji huru ambaye katika dirisha dogo la usajili alisajiliwa na Lipuli FC ya Iringa ambayo ameshaanza kuitumikia katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.

JUMA LIUZIO

Mwaka 2014 alisajiliwa na Zesco United ya nchini Zambia ambapo alicheza zaidi ya misimu miwili na mwaka 2017 aliamua kurudi kucheza soka nyumbani akisajiliwa na Simba. Alikaa hapo kwa mwaka mmoja kabla ya kusajiliwa na Mtibwa Sugar ambako yupo mpaka sasa.

JAMAL MWAMBELEKO

Baada ya kuvunja mkataba wake na Simba alisajiliwa Singida United, kwa muda wa mwaka mmoja lakini hakudumu hapo kutokana na kutopewa stahiki zake alikwenda katika timu ya KCB ya nchini Kenya ambayo aliitumikia kwa mwaka mmoja tu msimu wa 2018-19 na sasa amerudi nchini yupo katika klabu ya Namungo FC ambayo ilimsajili katika dirisha dogo.

MANYIKA PETER ‘JUNIOR’

Msimu uliopita alikuwa katika klabu ya KCB ya Ligi Kuu Kenya, lakini alicheza kwa msimu mmoja wa 2018-19 na msimu huu katika dirisha dogo amerudi nchini, na amesajiliwa na timu ya Polisi Tanzani ambayo ameanza kuitumikia.

MARCEL KAHEZA

Baada ya kusajiliwa na Simba akitokea Majimaji msimu wa 2017-18, hakucheza kwa muda mrefu kwani alitolewa kwa mkopo katika timu ya AFC Leopards ya Kenya mwaka 2018-19, na baada ya msimu huo kumalizika amerudi tena nchini na kwa sasa yupo katika klabu ya Polisi Tanzania.

TARIQ SEIF

Awali alikuwa akicheza soka hapa nchini katika timu za Stand United na Biashara United ambao baada ya mkataba wake kumalizika alikwenda kucheza soka la kulipwa nchini Misri katika timu ya Dekernes FC, huko alikaa kwa miezi sita tu na sasa amerudi nchini akisajiliwa na Yanga katika dirisha dogo kwa mkataba wa miezi sita.

Henry Joseph

EKiungo wa Mtibwa Sugar kwa sasa aliyetamba akiwa na Simba na baadaye mwaka 2006 aliuzwa Kongsvinger FC inayoshiriki Ligi Kuu nchini Norway na alicheza kwa mafanikio katika kipindi cha miaka minne. Baada ya hapo alirudi nyumbani na kuendelea kuichezea Simba japo safari hii hakuweza kudumu kutokana na kiwango na umri wake kumtupa mkono, na msimu ulipomalizika aliweza kuwekwa pembeni na nafasi yake kuchukuliwa na vijana Jonas Mkude na Said Ndemla.

Danny Mrwanda

Msimu wa 2008–09, Simba walimuuza katika timu ya Al Tadamon ya nchini Kuwait, ambapo alicheza msimu mmoja na kurudi tena Simba msimu wa 2009–10, baada ya hapo akaondoka na kwenda katika timu ya Dong Tam Long An ya nchini Vietnam ambapo alicheza hapo kwa msimu mmoja tu 2010–11. Msimu wa 2011, alijiunga na timu ya Hoàng Anh Gia Lai ya nchini humo humo lakini mwisho wa msimu aliondoka na kupita katika nchi mbalimbali na mwisho wa siku amerudi nchini na sasa yupo katika timu ya Mbeya Kwanza ya Ligi Daraja La Kwanza.

UHURU SELEMANI

AMshambuliaji wa zamani wa Simba, alisaini mkataba wa miaka miwili kuichezea klabu ya Jomo Cosmos mwaka 2015, ambayo ilipanda kucheza Ligi Kuu ya Afrika Kusini lakini baada ya muda alirudi tena kucheza soka nchini katika timu ya Biashara United. Ukiondoa Nizar Khalfan aliyecheza kwa muda Vancouver White Caps ya Canada kisha kurudi na sasa yupo pamba FC ya Mwanza, kicha akarudi. Alikuwa hakosekani kwenye wapo waliowahi kufanya majaribio au kusajiliwa lakini wameamua kurudi tena nchini ambao ni pamoja na Kelvin Sabato ‘Kongwe’, Hussein Sharif ‘Cassilas’, Yahya Zayd, Said Ndemla na Jonas Mkude.