Ni usiku wa wababe Ulaya

Muktasari:

  • PSG haitakuwa na Neymar wala Edinson Cavani, huku kukitajwa kuwapo na majeruhi wengine muhimu kwenye kikosi hicho cha Thomas Tuchel, lakini Lizarazu anaamini Mbappe atafanya kazi yake Old Trafford.

LONDON, ENGLAND.HAYA walete walete. Ule usiku wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ndo usharudi hivyo, huku macho ya wengi na masikio yakielekezwa huko Old Trafford leo Jumanne pale Manchester United itakapokuwa wenyeji wa mabingwa wa Ufaransa, Paris Saint-Germain.

Katika mchezo huo, PSG itakosa mastaa wake muhimu katika safu ya ushambuliaji, lakini staa wa zamani wa Ufaransa, Bixente Lizarazu anasema kwamba Kylian Mbappe peke yake atawatosha Man United.

PSG haitakuwa na Neymar wala Edinson Cavani, huku kukitajwa kuwapo na majeruhi wengine muhimu kwenye kikosi hicho cha Thomas Tuchel, lakini Lizarazu anaamini Mbappe atafanya kazi yake Old Trafford.

“Naamini anaweza kufanya uamuzi wa matokeo. Shida pekee inayomkabili kama atapewa pasi tu. Atapigiwa pasi? Hilo ndilo swali la kujiuliza. (Julian) Draxler au (Angel) Di Maria, wanapaswa kutimiza tu wajibu wao wa kumpa mipira sahihi,” alisema.

PSG inawafanya Man United kwa sasa ikiwa kwenye ubora wao huku ikiwa hawana shida ya majeruhi kikosini kwao jambo linalowapa jeuri ya kutamba. Lakini, mechi hiyo ni mtihani mzito kwa kocha Ole Gunnar Solskjaer, ambaye atakuwa na kazi moja ya kuhakikisha anaendelea kugawa dozi zake kwa wapinzani. Mechi nyingine itakayopigwa leo, Wataliano AS Roma wao watakuwa nyumbani kuwakaribisha Wareno FC Porto.

Kesho Jumatano, Ajax itakuwa wenyeji wa Real Madrid huku mechi hiyo ikionekana kama ya upande mmoja kutokana na rekodi nzuri za Los Blancos wanapocheza dhidi ya Wadachi hao, huku Waingereza Tottenham Hotspur itakuwa kwenye shughuli pevu ya kuwakabili Borussia Dortmund iliopo kwenye fomu yao kwa sasa huko kwenye Bundesliga. Kipute hicho kitafanyika Wembley na ripoti zinadai mambo yanaweza kuwa mazuri kwa Spurs kwani Marco Reus anahofiwa kuwa ni majeruhi na anaweza kukosa mechi hiyo jambo linalowapa unafuu.