SIMKOKO : Ni balaa! aanika sababu za ndumba viwanjani Ligi Kuu

Muktasari:

Tiririka naye katika mfululizo wa makala haya ya kocha huyo aliyewahi kutamba na klabu mbalimbali ikiwamo Reli Morogoro na Mtibwa Sugar.

NAAMUA kufunga safari ndefu kutoka jijini la Dar es Salaam hadi mji kasoro bahari, Morogoro. Ni umbali wa zaidi ya kilomita 190 ambazo zinautafuna muda wangu kwa saa 4 na ushei.

Ndio hivyo, dunia inabadilika! Miaka michache iliyopita kabla ya kuwepo haya mambo ya tochi barabarani, umbali huo tulikuwa tunaukata kwa saa 2:30 kwa kutumia mabasi ya Saddiq Line, Islam, Abood ama Hood.

Lakini kwa sasa madereva wanaendesha kwa mwendo kinyonga kwani ukienda mwendo kasi, tochi inakusoma na kupigwa faini. Hii ndio maana inatuchukua saa 4 na kitu kwenda ama kurudi Dar mpaka Moro. Maisha yamebadilika mno!

Licha ya mwendo huo kuchosha, lakini kiu niliyokuwa nayo juu ya safari hiyo ya Morogoro wala sikuijali. Niliona ni kama natoka Mbezi kwenda Gongo la Mboto ama Mbagala katikati ya foleni zilizopo kila barabara za jiji la Dar es Salaam.

Nafika salama mjini Morogoro na moja kwa moja nafunga safari fupi hadi Uwanja wa Jamhuri. Ndio, nilikuwa nimeshawasiliana na mwenyeji wangu, aliyeniambia nikutane naye hapo.

Nafika na kukutana na mwenyeji wangu. Ilikuwa majira ya alasiri hivi wakati nakutana mtu huyu aliyepanda hewani na akiwa na mwili unaonyesha ukakamavu katikati ya umri unaokadiriwa zaidi ya 60. Nasalimiana naye na kujitambulisha kwake kwa mara nyingine, naye ananikaribisha ndani ya ofisi yake iliyopo uwanjani hapo. Alitaka tufanye mahojiano naye kwa haraka kwani jioni yake alitarajiwa kuwa na pilikapilika za kusimamia mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Ndio, mechi hiyo ilikuwa ichezwe kwenye Uwanja wa Jamhuri, anaousimamia kama meneja wake. Wenyeji Mawenzi Market walikuwa wakiikaribisha Namungo. Mechi hii ni kati ya zile zilizoipa Namungo tiketi ya kupanda Ligi Kuu Bara.

Huyu si mwingine bali ni Mkufunzi na Kocha maarufu wa soka nchini, John Reuben Simkoko.

Kocha huyo anayeshikilia rekodi iliyoshindwa kuvunjwa kwa muda mrefu anafanya mahojiano maalum na Mwanaspoti na kufunguka mambo mengi ikiwamo rekodi yake aliyoiweka miaka 20 iliyopita.

Tiririka naye katika mfululizo wa makala haya ya kocha huyo aliyewahi kutamba na klabu mbalimbali ikiwamo Reli Morogoro na Mtibwa Sugar.

WAZAWA WANAKWAMIA WAPI?

Awali ya yote baada ya kunipa wasifu wake namuuliza kitu gani kinakwamisha makocha wazawa kushindwa kuaminiwa na klabu nyingi nchini kwa sasa, tofauti na ilivyokuwa zamani.

Nalazimika kuuliza hivyo kwani inaoonyesha mpaka sasa hakuna kocha yeyote mzawa aliyewahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara tangu Simkoko alipotwaa mara mbili mfululizo mwaka 1999 na 2000.

Anajikohoza na kujibu kwa upole; “Zipo sababu nyingi zinazofelisha makocha wazawa, lakini moja ni kukosekana ule uzalendo wa kumtayarisha mtu kwa tukio kama hilo.”

Anasema makocha wazawa hawathaminiwi na viongozi wa klabu, lakini pia huwa hawapewi muda wa kukaa muda mrefu ndani ya timu ili kutengeneza kikosi cha ushindi.

“Hata wachezaji hawakai muda mrefu pamoja, hilo linawapa ugumu makocha, na pia wenyewe (makocha) hawathaminiwi na klabu ndio maana hawadumu klabu moja kwa muda mrefu.”

“Ukiangalia mafanikio ya timu yangu ya awali kuzalisha vipaji ya Reli Moro nilikuwa nayo zaidi miaka sita hadi kufikia mafanikio yake, niliwajenga vizuri na kusajili pia vizuri,” anasema.

Anasema kukaa na timu kwa muda mrefu kulimpa nafasi ya kuchagua wachezaji wazuri kwa kushirikiana na viongozi wa timu ambao nao walikuwa wanamichezo, na kusisitiza kocha anapokuwa na timu kwa muda mrefu ni rahisi kujenga kikosi imara.

Anaongeza hata alipokuwa Mtibwa Sugar nako alikaa nayo zaidi ya miaka sita na aliweza kutengeneza timu yenye ushindani na kupata mafanikio ambayo yamebaki historia hadi leo nchini.

“Kukaa na timu hiyo kwa muda huu mafanikio yake yalionekana, kwani nilichukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara mara mbili mfululizo na kushinda pia vikombe vingine kama Kombe la Jiji la Mombasa kwa kuzifunga timu zote za Kenya.”

Anasema kocha anapokaa na timu kwa muda mrefu humpa nafasi ya kujitathimini mwenyewe yupo katika kiwango gani, anahitaji mchezaji wa aina gani.

“Kocha kukaa kwa muda mfupi katika timu hakuwezi kumpa nafasi ya kujenga timu, ndio maana mara zote wanaonekana hawafai,” anasema.

UBABAISHAJI MTUPU

Simkoko anasema jambo la pili linalowakwamisha makocha wazawa ni ubabaishaji walionao viongozi wengi wa soka ambao asilimia kubwa hawana ujuzi wa mchezo huo.

Anasema wengi wa michezo katika zama hili sio wanamichezo, bali ni watu waliojipenyeza michezoni kwa ajili ya kusaka umaarufu na masilahi na ndio wanaowavuruga.

Pia anasema hata elimu ya makocha nayo ni tatizo na kuna baadhi ya viongozi huchanganya kuhusu suala la sheria za soka na bahari kwa kufafanua kocha anaweza kuwa hana elimu akafanya vizuri.

Lakini pia kocha akawa na elimu na asifanye vizuri na hapo ndio viongozi wanapoyumba na kukimbilia zaidi kutafuta makocha wenye bahati na sio wenye taaluma ili watengeneze timu na kufeli.

Simkoko anasema kwa mantiki hiyo inategemea historia ya kocha husika elimu yake ameichukulia wapi na amekuwa mtu wa michezo kwa muda gani, lakini bado anadai kuwa si kweli kocha nzuri ni lazima awe umecheza soka kwa kiwango cha juu, ila kuucheza kuna faida yake katika kufundisha mpira mwenyewe.

“Faida ya kucheza soka kwa kiwango cha juu kunasaidia kumpa heshima kocha kwa wachezaji wake, ni rahisi kuongea lugha moja na wachezaji wake,” anasemea na kufafanua;

“Jambo jingine uzoefu wake unamsaidia katika ufundishaji wa mpira kwa wachezaji, japo kwa sasa elimu imekuwa juu sana lakini changamoto kubwa kwa makocha wa sasa ni ishu ya mikataba.”

MIKATABA YA OVYO

Simkoko anasema mikataba wanaopewa makocha ni ya muda mfupi sana, kiasi imeshakuwa ni kama fasheni tu, kocha kupewa mkataba wa kufundisha kwa miezi sita au mwaka mmoja.

“Hii si rahisi kuwa na kiwango bora kwa timu kwa kocha mwenye mkataba wa aina hii. Bahati mbaya makocha nao wamekuwa wakikubali kwa sababu ya shida wanazokuwa nazo.”

Anasema mkataba wa muda mfupi haumpi kocha nafasi ya kutengeneza mipango ya muda mrefu, anatengeneza zaidi kupata matokeo ili aongezewe dili kwani muda uliopo ni vigumu kufanikisha.

“Kwa kukimbizana na muda na kutaka kufanya mambo kwa haraka ili kuridhisha mabosi, makocha hujikuta wakikwama na kuachwa akionekana kafeli, hii ni mikataba ya ovyo.

“Mpira si kitu rahisi ni mipango ya muda mrefu na una hesabu zake, mpaka upate jibu kuna mambo mengi sana kumjengea mtu thamani, mchezaji umkubali na akubalike na watazamaji ni hatua kubwa,” anafafanua.

Simkoko anasema kwa kifupi ni kwamba makocha wazawa hawakubaliki kwa viongozi na hata mashabiki wa soka, ndio maana wamekuwa wakichukuliwa poa na kutukuzwa wageni.

Anasema hilo lipo hata kwenye suala la malipo ya mishahara na kutekelezewa mahitaji yake kiufundi, anasema wageni wanasikilizwa na kupewa kila wanalotaka, lakini sio kwa wazawa.

“Hata vitabu vya dini zinasema Nabii huwa hakubaliki kwao, makocha wazawa hawathaminiwi, japo inategemea na wenyewe wanavojiweka na kujenga thamani yake anapoingia makubaliano.”

NINI KIFANYIKE?

Simkoko anasema imefika wakati makocha wazawa wajithamini kwanza ndipo wathaminiwe, lakini pia wasipende kujirahisha na ikiwezekana watoke nje ya nchi ili kujenga majina yao.

Anasema kukubali kwao kuchukuliwa kama makocha wa muda ama wasaidizi tu kunawashushia heshima mbele ya viongozi, wachezaji na wadau wengine na mwishowe kudharauliwa.

“Sio kama Tanzania hakuna makocha wazawa wenye kiwango cha juu na wenye uwezo wa kuzisaidia timu, ila wenyewe hawajitambui na wala kujithamini, ndio maana wanachukuliwa kirahisi.” anasema.

USHIRIKINA KATIKA SOKA

Simkoko anakiri katika soka masuala ya ushirikina yapo na yamekuwa yakifanyika sana kwenye klabu nyingi, lakini kwa mtazamo wake haamini kama unasaidia lolote.

“Haya ni masuala ya mila na utamaduni tu wa Kiafrika, wakati mwingine hutumiwa kama njia ya kuwajenga kisaikolojia wachezaji, ila ukweli hayana tija na sijawahi kuyaamini katika umri wangu.”

“Ujue mambo ya kitamaduni yana nyanja nyingi, kuna watu wanajitibu kitamaduni, ni suala la kiimani lakini mimi siamini hilo kwangu halina nafasi lakini siwezi kugombana na anayeamini hivyo.”

Anasema kwa uzoefu alionao katika ukocha wa soka huwa vigumu kumzuia mchezaji au kiongozi wa timu wenye imani hizo kwani ni imani yake na kuna wakati hata kocha anashirikishwa kulingana na misimamo na imani yake.

Kwake anaamini timu inahitaji maandalizi mazuri ya kuwajenga wachezaji kisaikolojia, kuwa tayari kwa mchezo lakini si kutegemea ushirikina akidai bila maandalizi na kujituma uwanjani hakuna matokeo mazuri katika soka.

“Ushindi kwa timu ni kumtimizia mchezaji na kocha mahitaji yake, nakumbuka wakati nikiwa Mtibwa Sugar walikuwa makini sana kwa kuwatimizia mahitaji ya wachezaji, posho, motisha kwa wachezaji hivyo wachezaji walikuwa wanatimiza majukumu yao.”

Usikose Mwanaspoti kesho Jumanne uone kinachomnyima usingizi Ligi Kuu.