Ni Ligi ya Simba na Yanga tena

Muktasari:

Matokeo yake ni Watanzania wengi wamepoteza shauku iliyokuwepo siku za nyuma na kusababisha idadi ya watazamaji kupungua, ukiachilia michezo michache kama kati ya watani wa jadi, Yanga na Simba, wanapokutana.

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara utafunguliwa kesho kwa mechi ya Ngao ya Jamii kati ya mabingwa wa Ligi Kuu Simba dhidi ya mabingwa wa Kombe la Shirikisho Azam FC, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Wakati miamba hiyo ikijiandaa kutoana jasho kesho, bado Shirikisho la Soka (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) hawajaweka wazi kanuni za ligi hiyo ambayo inasemekana huenda timu zaidi ya nne zikashuka daraja mwisho wa msimu huu ili ligi iwe na timu 16 msimu ujao.

Ukimya wa TFF/TPLB katika jambo hilo, unaziweka njiapanda klabu shiriki pamoja na wadau wote wa soka nchini huku pia bado kukiwa na giza kuhusu suala la mdhamini mkuu kama amepatikana ama hajapatikana kama ilivyokuwa msimu uliopita ambao uliendeshwa kiugumu ugumu bila ya pesa za udhamini.

Kuna mengi ya kufanywa ili ligi msimu huu iwe bora.

Kwa mtazamo wangu ligi ina matatizo mengi ya mfumo na uongozi na badala ya kila msimu kuwa bora zaidi tunapiga hatua moja nyuma.

Matokeo yake ni Watanzania wengi wamepoteza shauku iliyokuwepo siku za nyuma na kusababisha idadi ya watazamaji kupungua, ukiachilia michezo michache kama kati ya watani wa jadi, Yanga na Simba, wanapokutana.

Siku hizi baadhi ya michezo inavutia watazamaji wachache na mashabiki wengi wanajitambulisha na kufuatilia ligi za Ulaya, hasa ya England.

Hata watoto wadogo wanajuwa zaidi habari za klabu na wachezaji na makocha wa timu za Uingereza, Hispania, Italia, Ujerumani na nchi za Amerika ya Kusini kuliko za klabu na wachezaji na walimu wa nyumbani.

Sababu zilizotufikisha hapa ni nyingi na unaweza kusema zinajaza kikapu. Kwa bahati mbaya viongozi wa Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF) wanaonekana kuzifumbia macho kama hawana habari nazo.

Kwanza nadhani kuwa na timu nyingi ni dosari kwa vile sio tu mechi ni nyingi na zinawachosha wachezaji, hasa kwa vile wanatumia muda mrefu katika safari kutokana na ukubwa wa nchi yetu.

Mfumo wa sasa wa kuwa na timu 20 zilizotapakaa kila pembe ya nchi unaonekana kupunguza mvuto.

Gharama za klabu kuweza kushiriki vizuri ni mzigo usiobebeka kutokana zaidi na shida ya kuwapata wadhamini ambao wakijitokeza hupendelea zaidi kusaidia klabu ‘kubwa’.

Klabu ndogo za mikoani zilizojitutumua na hata kuishiwa nguvu zilipoweza kupanda ngazi kwa shida hujikongoja huku zikiwa na hali ngumu na kushiriki kwao huwa zaidi kutaka zisiporomoke na kurudi zilikotoka.

Ni vizuri idadi ikapunguzwa na kuwa 16 na zicheze katika makundi mawili, kila moja liwe na timu nane na timu nne kutoka kila kundi ziingie hatua ya mwisho itayojumuisha timu 8 kutafuta mabingwa.

Mfumo wa aina hii unatumika katika nchi nyingi zenye ukubwa kama wa Tanzania.

Jambo jingine linalofaa kumulikwa ni la udhamini. Ni vizuri kutafuta wadhamini wawili, watatu au zaidi na mashirika ya umma yashajiishwe kuona yanao wajibu wa kuchangia kuendeleza kandanda nchini.

Uzoefu wa miaka ya karibuni umeonyesha kutegemea mdhamini mmoja unaiweka Ligi Kuu rehani kwa mdhamini kujifanya ndiye mwenye hati miliki na kuwa na uhuru mkubwa wa kuiendesha kama shamba lake.

Tumeona pia timu zinasajili wachezaji wengi na matokeo yake wengi huwa muda wote wamekaa kwenye mabao kama watazamaji. Hili nalo liangaliwe kwa makini.

Kutokana na msisimko, watazamaji wanakuwa wachache kuliko tunavyoona kwa baadhi ya mechi za mitaani maarufu kama Ndondo Cup, au soka la watoto wadogo katika viwanja vya mtaaani na vijijini.

Kwa hili inafaa TFF kutafuta njia za kuvutia watazamaji . Miongoni mwao ni kupunguza ada za malipo na kubadili mfumo wa mshindi kuondoka na alama tatu na timu zinapotoka sare kila moja kupata alama moja.

Badala yake mshindi abebe kitita cha pointi nne na timu zikitoka sare

kila moja ipate alama moja. Hii itazifanya timu zinazoshiriki kuwa na shauku kubwa ya kutafuta magoli, jambo ambalo ndio mashabiki wengi wanalitaka wanapokwenda uwanjani.

Njia nyingine inayoweza kuvutia watamaji zaidi ni kuanzisha mpango wa kuwa na mashindano ya mbio za masafa mafupi (mita 100 na 200) wakati wa mapumziko badala ya watazamaji kukaa dakika 15 wakisubiri timu zirudi uwanjani kwa ngwe ya lala salama.

Jambo jingine lisililofaa kurejewa kwa kisingizio chochote kile ni kwa timu moja au mbili kuwa na viporo vitatu au vinne vya mechi.

Ratiba lazima ihakikishe hapana timu inayokuwa na zaidi ya kiporo kimoja ili kuepuka lawama za kuwepo mpango wa kuipa timu yoyote ile nafasi nzuri ya kuibuka bingwa kirahisi.

Katika nchi nyingi siku hizi mtindo wa zamani wa wageni wa heshima katika michezo kuwa viongozi (mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya au madiwani) umewekwa kando.

Badala yake wachezaji mashuhuri wa zamani, wake au watoto wao, ndio hupewa heshima hio na siku hiyo mchango mkubwa wa huyo mchezaji kwa taifa hutolewa maelezo na kuvutia watazamaji.

Nadhani vizuri na sisi tukafanya hivyo kwani itawapa ari wachezaji wetu kuona watavyothaminiwa wataostaafu kama wanavyofanyiwa wenzao waliowatangulia.

Fikiria hali itakuwaje uwanjani wachezaji walioipatia heshima nchi hii katika michezo kama Peter Tino (kandanda) au Filbert Bayi aliyeweka

rekodi ya dunia ya mita 1,500 kuwa ndiye mgeni wa heshima badala ya diwani ambaye hata siku moja hajaiwakilisha nchi katika mchezo wowote ule.

Mchezo wa kandanda umepitia mageuzi mengi ya sheria, kanuni, kivazi na mfumo wa mchezo.Sio vibaya na sisi kufanya mageuzi ambayo hayatapindua sheria za mchezo.

Kinachohitajika ni kuwa wabunifu ili kuleta msisimko wa mchezo na hatimaye kuwa taifa lenye kuheshimika katika kandanda badala ya kuendelea kuwa wasindikizaji badala ya washindani katika medani ya kimataifa.

Tusiogope mageuzi na tuanze kwa msimu ujao. Vyenginevyo tutabaki tunasikitika kuona wakati nchi ndogo kama Comoro, Cape Verde na

Burkina Faso zimeweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo ya soka na sisi sio tu tunabakia tulipokuwa bali tunarudi nyuma.

Tuyatafute mageuzi yatakayotupa maendeleo sasa vinginevyo tutaendelea kuzishuhudia timu zenye uwezo binafsi wa kifedha za Simba na Yanga na Azam tu zikiendelea kutawala ligi hii bila ya kupata ushindani wa kweli kutoka kwa timu nyingine ndogo.