Ni Lamine na Mwamnyeto tu

Wednesday September 16 2020

 

By OLIVER ALBERT

KWA mujibu wa Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ Kocha wa Yanga, Zlatko Krmpotic asipangue kabisa ukuta wa Lamine Moro na Bakari Mwanyeto pale kati maana haupitiki.

Beki huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, jamaa ni watu wa kazi kweli kweli na ndio wanatakiwa kuendelea kucheza pamoja.

Malima alivutiwa na jinsi mabeki hao wawili walivyocheza kwa kiwango kikubwa katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City, ambao Yanga ilishinda 1-0 lililofungwa na Moro.

Beki huyo mwenye mwili mkubwa alisema Moro na Mwamnyeto wameonekana kutengeneza safu nzuri ya ulinzi na ambayo itakuwa haipitiki kirahisi kutokana na ubora na akili waliyonayo wachezaji hao.

“Nakumbuka mechi ya siku ya Mwananchi walicheza Mwamnyeto na Abdallah Shaibu’Ninja’, kisha mechi ya Prisons wakacheza tena hao wawili na mechi ya Mbeya City ndio Moro akarejea.

“Ukiangalia kombinesheni hizo mbili, kombinesheni ya Moro na Mwamnyeto imeonekana kuwa vizuri zaidi. Kwani Mwamnyeto ni mmoja ya mabeki wazuri na katika usajili mzuri ambao Yanga wamefanya msimu huu, basi huo ni mmoja yule ndio aina ya mabeki wanaotakiwa Yanga.

Advertisement

“Wakiendelea kucheza pamoja na Moro, beki ya Yanga itaendelea kutulia sana kwani wote wanacheza kwa akili na wana mawasiliano mazuri wakati wakiwa uwanjani ili kutochanganyana katika kutimiza majukumu yao’, alisema Malima.

Malima alisema Yanga ya msimu huu imetulia kwani kila nafasi ina wachezaji zaidi ya wawili hivyo kuongeza ushindani katika kikosi hicho utakaowasaidia kufanya vizuri.

“Kwa sasa ni ngumu kujipa matumaini Yanga inaweza kushinda mabao mengi katika mechi zake za ligi kwa sababu bado timu haina muunganiko mzuri.

“Hivi sasa Yanga inatengeneza timu na jambo baya kocha alikuja kujiunga na kikosi hicho siku chache kabla ya kuanza ligi hivyo bado yuko katika harakati za kutafuta muunganiko wa timu yake. Hivyo mpaka labda kuanzia mechi ya tisa au 10 ndio watu wataanza kuuona moto wa Yanga kwani tayari wachezaji wote watakuwa wamezoeana”, alisema Malima.

Advertisement