Ngoma droo: Si Ole Gunnar Solskjaer wala Pochettino

Muktasari:

Mwisho wa siku United itaendelea kucheza kamari tu kwa makocha mpaka atakapopatikana kocha ambaye atafuata nyayo za Sir Alex Ferguson. Kibarua hiki kimekuwa kigumu sana pale Old Trafford.

ED Woodward, katika ofisi moja ya mabosi zake, pale New York Marekani au Dubai, au popote duniani, atakuwa anatazamana na mabosi wake matajiri familia ya Grazer Mei mwaka huu kujadili habari nzito. Nani awe kocha ajaye wa Manchester United?

Kwa sasa jibu linaweza kuwa rahisi. Ole Gunnar Solskjaer. Jibu rahisi sana kwa sasa. Ametoka sare moja tu katika mechi zote alizoisimamia timu hiyo tangu aichukue kwa Jose Mourinho siku chache kabla dunia haijala pilau ya Krismasi mwaka jana.

Mabosi wake watakuja sura. Kwanini Ole Gunnar? Jibu lake litakuwa jinsi ambavyo aliibadili timu baada ya kuikuta hoi katika mikono ya Jose Mourinho. alikuta hakuna matokeo uwanjani. Nje ya uwanja alikuta Jose haongei na Paul Pogba, haongei na Luke Shaw vema, haongei na Anthony Martial vema, haongei na wachezaji wengi vema.

Sasa hivi yeye anaongea nao vema. Sasa hivi chini yake timu yake inashinda. Inaweza kuwa sababu ya kumpa timu. kwa mtazamo wangu hapana. Timu ambayo inatoka kwa kocha mkorofi kwenda kwa kocha mwingine ina nafasi ya kupata matokeo mazuri.

Ghafla wachezaji wote wanajikuta na furaha ya ajabu. Ghafla wote wanataka kuthibitisha kwamba wao sio tatizo bali kocha aliyeondoka ndiye tatizo. Kila kitu kinabadilika klabuni na mgeni mpya anaonekana ana maajabu.

Ikifika msimu ujao, maisha yaanza upya. Binadamu wanarudi katika ubinadamu wao. Ile morali inaweza kuyeyuka kwa sababu watu wanaanza kuzoea mabadiliko. Mazoea yanarudi. Hapa ndipo Solskjaer anapoweza kujikuta katika wakati mgumu.

Iliwatokea Chelsea. Machi 2012 walipomfukuza Mreno mwingine, Anre Villas-Boas walimchagua Roberto Di Matteo kuwa kocha wao wa muda. Ghafla akabadili kila kitu. Wakachukua FA na kisha wakachukua ubingwa wa Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia yao na historia ya timu za London.

mwishoni mwa msimu walimchagua kuwa kocha wa kudumu. Alidumu kwa miezi minne tu. alifukuzwa Novemba 2012. Kisa? Matokeo mabovu. Kwanini? Inaweza kuwa wachezaji walipandisha morali alipoingia yeye, halafu katika msimu uliofuata wakarudi katika mazoea ya kawaida.

Hiki ndicho ambacho kinaweza kumtokea Solskjaer? Nadhani matajiri wa United pamoja na watu wengine wa bodi wanaweza kumpa Woodward kuhusu mfano huu wa Di Matteo. Sijui atawaambia nini. Inawezekana ndio maana kuna watu ndani ya United bado wanataka Mauricio Pochettino wa Tottenham apewe kiti hicho bila ya kujali kile ambacho Solskjaer anakifanya kwa sasa.

Lakini kwa Pochettino mwenyewe bado kuna maswali mengi. Kwanini jina lake ni maarufu kwa timu kubwa? Kwa sababu ameweza kuitengeneza Spurs kuwa timu imara bila ya kutumia pesa nyingi. Kwa misimu miwili mfululizo Spurs imekaa katika Top Four.

Huu ni msimu wa tatu mfululizo Spurs inawania ubingwa huku ikiwa imetulia Top Four na safari hii wamefanya hivi bila ya kutumia pesa yoyote katika madirisha mawili ya uhamisho yaliyopita. Hawakununua mchezaji katika dirisha kubwa la mwaka jana na wala hawakununua mchezaji katika dirisha la Januari. Sana sana wamemruhusu Moussa Dembele kwenda China.

Pochettino anaonekana kufanya maajabu. Manchester United wanamtamani na Real Madrid wanamtaka. Kinachoonekana katika hisia za wanaomtaka ni kwamba Pochettino akiongezewa pesa kidogo basi anaweza kufanya maajabu makubwa kuliko haya anayoyafanya sasa hivi Spurs.

Tatizo ni moja, Pochettino hajawahi kutwaa taji lolote kama kocha katika maisha ya kazi hiyo. Akiwa na Espanyol, Southampton na kisha sasa hivi pale Spurs hajawahi kutwaa taji lolote. Ana mbinu za kushinda mataji au kuiimarisha timu tu? hili ndio swali.

Akipewa nafasi kisha akapewa pesa, kuna uhakika wowote kwamba ana uwezo wa kuigeuza klabu yako kuwa ya mataji? Bado haina uhakika sana. hajawahi kufanya hivyo hapo kabla. Ndio maana bado inabakia kuwa bahati Nasibu tu.

Kwa United kumchukua Ole Gunnar au Pochettino bado ni kitu cha bahati nasibu tu. lakini hata hivyo sio mbaya kuwajaribu kwa sababu nje ya hao makocha wengi bora wana timu zao. Pep Guardiola ana timu yake, Jurgen Klopp ambaye amewahi kushinda kitu huko nyuma naye ana timu yake.

Mwisho wa siku wale wanaomtaka Ole Gunnar watakuwa na hoja zao na wale wanaomtaka Pochettino watakuwa na hoja zao.

Sijui Ed Woodward aralaza hoja gani mbele ya wajumbe katika kumuhalalisha mmoja kati ya Solskjaer au Pochettino.

Vyovyote ilivyo atapata upinzani mzito na hata majibu yake yakija nje yatapata upinzani mzito. Ukimchagua Solskjaer linaweza kuonekana kosa, ukimchagua Pochettino linaweza pia kuonekana kosa.

Mwisho wa siku United itaendelea kucheza kamari tu kwa makocha mpaka atakapopatikana kocha ambaye atafuata nyayo za Sir Alex Ferguson. Kibarua hiki kimekuwa kigumu sana pale Old Trafford.