Ngoma, Chirwa wampa jeuri Cioaba

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti, Cioaba alisema kwa kiasi kikubwa wachezaji wengi aliowaacha amekutana nao klabuni huku akisisitiza kuwa Azam ina kikosi kizuri kutokana na kuwa na mchezaji zaidi ya mmoja kwa kila nafasi.


ACHANA na matokeo ya juzi Jumanne kwenye mechi yao dhidi ya Simba katika mfululizo wa Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa Azam, Aristica Cioaba amesema amefurahia ongezeko la washambuliaji, Obrey Chirwa na Donald Ngoma katika kikosi chake.

Cioaba aliyeifundisha Azam misimu miwili iliyopita amerejea tena klabuni hapo kwa mkataba wa mwaka mmoja akipokea mikoba ya Etienne Ndayiragije ambaye anatarajia kuwa kocha mkuu wa Taifa Stars.

Akizungumza na Mwanaspoti, Cioaba alisema kwa kiasi kikubwa wachezaji wengi aliowaacha amekutana nao klabuni huku akisisitiza kuwa Azam ina kikosi kizuri kutokana na kuwa na mchezaji zaidi ya mmoja kwa kila nafasi.

“Aggrey Morris, Shaaban Chilunda, Mudathir Yahya, Frank Domayo na wachezaji wengine wengi nimewafundisha, kwa upande wa Ngoma na Chirwa ni wachezaji wazuri nilikuwa nawaona wakiwa Yanga kuongezwa Azam ni mpango mzuri,” alisema.

“Ukiachana na hao pia kuna ongezeko kubwa la nyota eneo la ushambuliaji, natarajia changamoto kutoka kwa wachezaji hao kuhakikisha napata kikosi bora cha ushindani na malengo niliyonayo ni kutwaa taji la ligi.”

Cioaba alisema uwepo wa wachezaji wengi kwenye nafasi moja unampunguzia changamoto ya kuwakosa baadhi yaokutokana na kuwa majeruhi na kujikuta anawabadilisha namba wachezaji wengine. Alisema ili kikosi kiwe imara na bora kinahitaji wachezaji wengi na wenye ushindani kwenye namba moja jambo ambalo analiona kwa Azam kutokana na wingi wa wachezaji.