Ngoma, Chirwa waachiwa msala

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti, Morris alisema safu ya ushambuliaji ndio itakayoamua nafasi ya timu hiyo kuendelea katika hatua inayofuata kwani wana deni la kulipa kwa wageni wao walioacharaza ugenini.

BEKI kisiki na nahodha wa Azam FC, Aggrey Morris amewaachia msala mastraika wao wa kigeni, Donald Ngoma na Obrey Chirwa akisema wao ndio wanaoshikilia hatma ya timu yao kuvuka raundi ya awali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Azam inaikaribisha Fesil Kemena ya Ethiopia baada ya mchezo wao wa kwanza ugenini kuchapwa bao 1-0 na kujiweka katika mazingira magumu kusonga mbele keshokutwa Jumamosi watakaporudiana na wapinzani wao hao kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Hata hivyo, nahodha huyo ambaye yupo nje ya uwanja kwa miezi karibu miwili tangu alipoumia kwenye mazoezi ya Taifa Stars iliyokuwa ikijiandaa na fainali za Afcon 2019, alisema Azam itafuzu kama kina Chirwa wataamua kufanya kweli nyumbani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Morris alisema safu ya ushambuliaji ndio itakayoamua nafasi ya timu hiyo kuendelea katika hatua inayofuata kwani wana deni la kulipa kwa wageni wao walioacharaza ugenini.

Alisema kikosi chao kimekamilika kila idara isipokuwa safu hiyo ya mbele bado haijaonyesha kuelewana pamoja na kuwa na washambuliaji wengi na kama keshokutwa watakuwa na macho ya kuona nyavu basi Azam haina sababu ya kukwama nyumbani.

“Azam hata kule ugenini safu hii ilikosa umakini, lakini tulikuwa na uwezo wa kuwafunga Kemena kwao, ila naamini Kocha atakuwa ameona tatizo la kurekebisha na sasa ni zamu ya washambuliaji kupambana, huku mabeki nao walinde lango kwa umakini.”

“Kama Ngoma, Chirwa au Idd Seleman ‘Nado’ atatumia nafasi watakazotengeneza basi watakuwa na kazi rahisi ya kuwaaminisha Watanzania kuwa wao ni bora na wanastahili kushiriki mashindano hayo kutokana na usajili walioufanya.”

Kuhusu hali yake kwa sasa alisema; “Naendelea vizuri na tayari nimeanza mazoezi mepesi kujiweka fiti nipo Zanzibar naiombea timu yangu iweze kupata matokeo mazuri ikiwa ni sambamba na wawakilishi wengine Tanzania katika michuano hiyo ya CAF.

Timu nyingine shiriki ni KMC inayocheza kesho dhidi ya AS Kigali ya Rwanda katika Kombe la Shirikisho, Malindi na KMKM za Zanzibar pamoja na vigogo Simba na Yanga zilizopo Ligi ya Mabingwa Afrika.