Ngasa aaga Yanga

Monday August 3 2020

 

By Mwandishi Wetu

SIKU chache baada ya dirisha la usajili kufunguliwa, mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngasa ameaga rasmi ndani ya klabu hiyo baada ya kuandika ujumbe kuwa hatakuwa miongoni mwa wachezaji wa timu hiyo msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Ngasa ameandika ujumbe huo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram akishukuru uwepo wake ndani ya Yanga.

Ngasa ameandika kuwa; "Kwanza nitowe shukrani zangu kwa wote tuliokuwa pamoja katika kipindi chote Yanga viongozi wangu mashabiki na wachezaji wenzangu kwa kikoo kilichofanyika leo, sitakuwa katika kikosi cha Yanga niwatakie mafanikio yalio mema, Enjoy soccer,"

Ngasa ameandika maneno hayo ikiwa ni muda mfupi kukutana na viongozi wake ambao leo Jumatatu Agosti 3, 2020 wamekutana na wachezaji wao wote kuwaambia mustakhabali wa maisha yao ndani ya Yanga.

Mshambuliaji huyo ambaye amewahi kuzichezea timu mbalimbali ikiwemo Azam, Simba, Free State ya Afrika Kusini, Kagera Sugar, Mbeya City na Ndanda FC mkataba wake pia umemalizika mwishoni mwa msimu huu.

Hivyo Ngasa ni miongoni mwa wachezaji ambao hawajaongezwa mkataba ndani ya Yanga huku wengine pia wakitarajiwa kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa.

Advertisement

Baada ya ujumbe wake huo, mashabiki wake wamtakia kila la kheri huku wengine wakionekana kusikitishwa kuondoka kwake.

Mwanaspoti itaendelea kukujuza wachezaji wote ambao wataachwa na klabu hiyo pamoja na wanaosajiliwa.

Advertisement