Neymar kuuzwa kwa bei ya hasara PSG

Friday July 12 2019

 

PARIS, UFARANSA. Paris Saint-Germain imeripotiwa kulegeza kamba na sasa ipo tayari kumpiga bei supastaa wao wa Kibrazili, Neymar kwa ada ya Pauni 135 milioni tu.

Mabingwa hao wa Ufaransa wapo tayari kufanya biashara hiyo katika dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya.

PSG wanaataka tu kuachana na mchezaji huyo baada ya kushindwa kuibuka mazoezini huku ikidaiwa kwamba huenda akakumbana na faini ya Pauni 340,000 kutokana na kitendo hicho cha kukacha kufika mazoezini.

Mpango wa Neymar, 27 ni kurudi zake kwenye timu yake ya zamani ya Barcelona. PSG licha ya kwamba walimnasa staa huyo kwa ada iliyoweka rekodi ya dunia ya Pauni 198 milioni Agosti 2017, lakini sasa wapo tayari kupata hasara ya Pauni 63 milioni.

Gazeti linaloongoza huko Ufaransa, El Pais linaripoti kwamba klabu hiyo ipo tayari kumaliza dili hilo na kumruhusu Neymar arudi Barcelona anakotaka kwenda.

Limeripotiwa pia uongozi wa PSG unaamini hadhi ya timu inadhaminiwa zaidi kwa hadhi kuliko hesabu za kipesa, hivyo wanaona ni bora tu kuachana na kitu ambacho kitawashushia hadhi yao.

Advertisement

Mkurugenzi wa michezo wa PSG, Leonardo alishaweka wazi mpango wa kumuuza Neymar akisema alipozungumza na Le Parisien: "Neymar anaweza kuondoka tu PSG kama itawekwa mezani ofa nzuri."

Na alipoulizwa kama Barcelona wamefanya nao mawasiliano juu ya usajili wa mchezaji huyo, Leonardo alisema: "Ndio."

PSG ilithibitisha mapema Jumatatu kwamba itampiga faini mchezaji wao huyo baada ya kushindwa kutokea mapema mazoezini. Lakini, baba wa mchezaji huyo, ambaye pia ni wakala wake, Neymar Sr, amedai kwamba klabu inafahamu wazi kwamba Neymar hawezi kurudi klabuni hadi Julai 26 kwa sababu ya kuwa na majukumu ya wadhamini wake.

Leonardo alisema klabu inafahamu kuhusu jambo hilo, lakini hakukuwa na makubaliano yoyote ya tarehe ya kurudi kwenye timu. Lakini, staa huyo wa zamani wa AC Milan, alisema ni jambo la wazi, Neymar ameshaiambia klabu kwamba anataka kuondoka. PSG bado haijapokea ofa rasmi, licha ya kukiri kuwasiliana na Barcelona.

Advertisement