Neymar anataka auzwe ila bado majeruhi

Muktasari:

Mwanasoka huyu mwaka huu ameandamwa na majeraha ya mara kwa mara ikiwamo jeraha la kwanza la kuvunjika kifupa cha mguu ambapo aliumia mwanzoni mwa Februari.

HATIMA ya uhamisho wa mshambuliaji wa Klabu ya PSG, Neymar Jr. aliye majeruhi bado haijaeleweka mpaka dakika hii kwani ombi lake la kutaka arudi katika klabu yake ya zamani ya Barcelona bado linasuasua.

Staa huyo mwishoni mwa mwezi uliopita ilimlazimu kujitoa katika timu ya taifa ya Brazil inayoshiriki michuano ya Copa Amerika kutokana na majeraha ya goti.

Neymar mwenye umri wa miaka 27 alipata majeraha hayo akiwa katika siku ya kwanza ya mazoezi ya timu ya taifa ambao ndiyo wenyeji wa michuano.

Alionekana akitoka nje huku akichechemea na kushika goti lake la kushoto, na kutoka nje ya uwanja uliopo pembeni ya jiji la Rio de Janeiro ujulikanao kama Granja Comary.

Majeraha hayo mapya ya goti ndiyo yaliyomfanya staa huyu kuwa nje ya mashindano yanayojumuisha mataifa ya Amerika Kusini.

Akiwa anauguza jeraha hilo, Neymar tayari ameweka wazi kwa rais wa klabu yake ya PSG kuwa anataka kuondoka na kwenda kucheza katika klabu inayompa hisia kuwa yuko nyumbani ambayo ni Barcelona.

Mwanasoka huyu mwaka huu ameandamwa na majeraha ya mara kwa mara ikiwamo jeraha la kwanza la kuvunjika kifupa cha mguu ambapo aliumia mwanzoni mwa Februari.

Alipona na kurudi uwanjani Aprili 27 na kufanikiwa kuichezea klabu yake ya PSG mechi nne tu na aliitwa katika timu yake ya taifa kujiandaa na mashindano hayo ya Copa Amerika.

Wakati akiendelea kuuguzwa jeraha, klabu ya Barcelona bila kujali hali yake, wako tayari kukaa mezani na kumwaga pesa kwa PSG ili kumrudisha mchezaji huyo. Taarifa ya daktari wa timu ya taifa ya Brazil, Dk Rodrigo Lasmar ilieleza kuwa Neymar alipata maumivu ya goti la kushoto mara baada ya kupiga mpira hali iliyoashiria kuwa amepata majeraha ya tishu laini katika goti. Ingawa haikuwekwa wazi zaidi undani wa jeraha hilo, siku ya leo nitalitazama aina ya majeraha hayo ya goti kwa jicho la kitabibu.

Neymar amejeruhi nini gotini?

Kwa kuwa alipiga shuti ni dhahiri amejeruhi nyuzi ya ligamenti iliyopo katikati ya goti ambayo huwa na kazi ya kuzuia mifupa ya goti isiende uelekeo hasi upande wa nyuma.

Kitabibu nyuzi hii inajulikana kama Anterior Cruciate Ligament, kifupi ACL, ndiyo mhimili mkuu wa ungio la goti ikiwa eneo la katikati ya goti ikiunganisha mfupa mkubwa wa paja na wa chini ya goti.

Kwa namna Neymar alivyokuwa anatoka uwanjani siku hiyo huku akichechemea na kusaidiwa kidogo na Dk Rodrigo ni ishara kuwa hayakuwa majeraha makubwa. Jeraha la ligamenti kama ni kubwa huainishwa kama la daraja la tatu inayohusisha kukatika pande mbili na kuachana au kukwanyuka katika mfupa uliojipachika.

Kwa kawaida majeraha ya ligamenti huainishwa katika aina tatu za majeraha. Aina ya kwanza huwa ni kujivuta kupita kiwango na aina ya pili ni kuchanika pasipo kuachana pande mbili.

Daraja la tatu huwa ni jeraha baya linalohitaji upasuaji kama sehemu ya matibabu, jambo linalochagia mchezaji kukaa nje ya uwanja muda mrefu akiuguza jeraha la upasuaji.

Jeraha hili huwa ni kubwa na huambatana na maumivu makali ukilinganisha na daraja la pili na la kwanza, ambalo mchezaji anaweza kupata maumivu ya kati na hata kuweza kutembea kwa kuchechemea. Daraja la tatu ya majeraha haya huweza kuchukua muda mrefu kupona na kurudi tena uwanjani kwani huchukua miezi 6-9 mpaka mwaka.

Neymar alifanyiwa vipimo muhimu ikiwamo picha ya MRI ambayo inatoa taswira nzuri juu ya vitu vilivyomo katika ungio la goti na kubaini ni jeraha la daraja la pili la ligamenti.

Kwanini wanasoka wanapata zaidi majeraha ya goti?

Majeraha ya goti ni vigumu kuepukwa hasa kwa wachezaji wa soka ambao wanashiriki mashindano yenye ushindani. Wanamichezo wanaocheza mpira wa miguu ndiyo wanaongoza kwa kupata majeraha ya aina hii wakifuatiwa na mpira wa kikapu na rugby. Majeraha ya goti yako katika tatu bora ya majeraha yanayoongoza katika soka.

Takwimu za majeraha ya michezo zinaonyesha karibu asilimia 70 ya mejaraha ya nyuzi za ACL huwa si kwa kufanyiwa faulu wala si kugongana na mpinzani, bali mchezaji mwenyewe kujijeruhi kwa kulipinda vibaya.

Nyuzi ngumu za ACL ziko kama herufi ‘X’ kazi yake ni kuzuia mifupa inayounda ungio la goti kutulia katika eneo lake na isiteleze kwenda upande wa nyuma ya goti na vile vile kuwezesha goti kujizungusha.

Ikumbukwe kuwa goti lina mijongea mikuu mitatu ikiwamo kunyooka, kupinda kutoka mbele kuja nyuma na kujizungusha. Hivyo basi uelekeo mwingine wowote nje ya hii huweza kusababisha majeraha.

Neymar alijijeruhi mwenyewe baada ya kupiga shuti hivyo ni dhahiri kuwa nguvu kubwa aliyotumia kupiga ilisababisha shinikizo kubwa katika nyuzi hiyo ya ligamenti na kuvutika kupita kiasi.

Vile vile upo uwezekano kuwa nyuzi iliwahi kupata majeraha ya ndani kwa ndani hapo awali kwani kwa namna alivyopiga ni upigaji wa kawaida wa mwanasoka, hakutumia nguvu nyingi.

Jeraha hili linaweza kumnyima dili?

Kwa kawaida klabu kubwa hasa za kulipwa huwa hazikununui kama utimamu wa mwili hauko sawa, lakini aina hii ya jeraha linapona mapema kikamilifu na hivyo halitaweza kumkosesha dili.

Pia kutokana na ubora wa Neymar jopo la wataalamu wa afya wa klabu itakayomhitaji inaweza kutathimini majeraha hayo iwapo yatakapona atacheza bila tatizo.