Ndikumana aapa hao AS Kigali hawachomoki

Saturday August 17 2019

 

By Mwandishi wetu

NAHODHA Msaidizi wa KMC, Yusuph Ndikumana amesema kwa mazoezi wanayopewa na Kocha wao, Jackson Mayanja anaamini kabisa AS Kigali haiwezi kupona watakapokanyaga Uwanja wa Uhuru kurudiana nao kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika wiki ijayo.

KMC ina kibarua cha kusaka ushindi ili isonge mbele dhidi ya Wanyarwanda hao waliotoka nao suluhu mjini Kigali wiki iliyopita, hasa ikizingatiwa wanakabiliwa na majeruhi karibu watano wakiwa ni washambuliaji na beki mmoja.

Hata hivyo, Ndikumana alisema wanataka kuweka historia kwa kufika mbali kwenye mashindano hayo, hivyo ni lazima wapambane kuhakikisha mchezo huo wanashinda.

“Ukiangalia mechi ya kwanza tulicheza vizuri na tukatengeneza nafasi nyingi ila hatukuweza kuzitumia ndio maana hatukupata bao,” alisema.

“Hivi sasa tunaendelea na mazoezi na kubwa ambalo kocha anaangalia ni hilo tatizo la umaliziaji kwani lazima tuhakikishe tunapata ushindi mnono.”

Kocha wa timu hiyo, Mayanja alisema kwa sasa ana kazi ya kujipanga kwa mchezo huo hasa baada ya idadi ya majeruhi kumtibulia kwani washambuliaji wake watano anaweza kuwakosa kwenye mechi ijayo.

Advertisement

Nyota hao ni Ramadhani Kapera, Salim Aiyee, James Msuva, Cliff Buyoya na Charles Illanfya, huku beki Abdallah Mfuko naye akiwa kwenye hatihati kwani ni majeruhi.

Advertisement