Ndemla apate mtetezi Stars

Sunday October 04 2020
ndemla pic

WAKATI wadau mbalimbali wakiendelea kujadili uteuzi wa baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars akiwamo Said Ndemla, aliyekuwa kocha wa Simba Abdallah ‘King’ Kibadeni, amepongeza kitendo cha Kocha Etienne Ndayiragije kumjumuisha kiungo huyo katika kikosi kitakachowavaa Burundi.

Ndayiragije anayeinoa Stars juzi alitangaza majina 25 ya nyota wake kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayopigwa Jumapili ijayo jijini Dar es Salaam na kumjumuisha Ndemla na Ditram Nchimbi wa Yanga na kusababisha baadhi ya wadau kuwaka wakisema hawakustahili, lakini Kibadeni amekuwa tofauti.

Kibadeni aliiambia Mwanaspoti kuitwa kwa kiungo huyo fundi ndani ya Stars ni sahihi kutokana na uwezo wake aliokuwa nao kwa sasa ndani ya klabu yake.

Alisema, tangu msimu huu kuanza ameshuhudia nyota huyo akionekana ndani ya Simba akipata nafasi ya kucheza tofauti na msimu uliopita hakuweza kupata nafasi ya kuonyesha mchango wake kwa timu.

“Mchezaji akiitwa Stars inategemea na namna alivyoonyesha kiwango katika timu yake kwangu naona ni sawa kuitwa kwa Ndemla. Yule kijana uwezo anao mkubwa sana, aendelee kujituma ni kiungo mzuri mno.” alisema Kibadeni.

Advertisement