Ndemla, Fei Toto viungo bora zaidi- Ndayiragije

Dar es Salaam. Kocha wa Taifa ya Stars, Etienne Ndayiragije amewasifu viungo Said Ndemla wa Simba na Feisal Salum (Yanga) kuwa ndiyo bora zaidi nchini katika wachezaji wa nafasi wanazocheza.

Ndayiragije alisema katika kikosi chake, Ndemla ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mbele pamoja na Fei Toto’ wa Yanga tofauti na wengine ambao mara nyingi hupenda kupiga pasi nyingi za pembeni na nyuma zisizo na faida.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ndayiragije alisema: “Mfano ile pasi kiungo wa Simba, Larry Bwalya aliyompa Meddie Kagere (juzi) akafunga iliwapita viungo na mbeki na kumkuta mfungaji, sasa vile ndivyo inavyotakiwa, siyo unakuta mchezaji anaonekana amepiga pasi nyingi, lakini ukimfuatilia unakuta ni za pembeni na nyuma.

“Mtu pekee anayeweza kutoa pasi kama ya Bwalya mara nyingi, ambaye tuko naye ni Ndemla na Fei Toto, hawa wanaweza pasi hizo.”

Ndayiragije alisema amekuwa akiwafuatilia wapinzani wake, Tunisia atakaokutana nao katika hatua ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika.

“Najua kuwa Oktoba 13 wanacheza na Nigeria katika mchezo wa kirafiki. Katika kuwafutilia najua wakiwa nyumbani wanakuwa hatari zaidi na kwa sasa inabebwa na wachezaji wake wengi wa nje, ambao wamerejea kucheza ligi yao ya nyumbani, alisema.

Aidha, alitetea uamuzi wake wa kuwaita baadhi ya wachezaji na kumuacha Farid Mussa wa Yanga.

“Huu ni mchezo wa kirafiki, watu lazima wajue hilo, hawa wa sasa ndiyo niliowaita na wengine wakati wao ukifika nitawaita pia. Watu wanahoji kuhusu Yassin Mustapha na Kibwana, lakini wajue kuwa Bryson David na Israel Patrick ana pasi nne za magoli, hao.

.