Ndanda kutesti mitambo Namungo

Wednesday June 3 2020

 

By Oliver Albert

Kocha wa Ndanda, Meja mstaafu Abdul Mingange amesema wanatarajia kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Namungo ili kujiweka vizuri na Ligi Kuu Bara.

Mingange amesema mechi hizo zitawasaidia kukiweka fiti kikosi chake kabla ya kuivaa Biashara United Juni 20 kwenye mchezo wa ligi utakaofanyika kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara.

Ndanda ilianza mazoezi juzi Jumatatu kujiandaa na michezo iliyobaki ya Ligi Kuu baada Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kuruhusu michezo kurejea kuanzia Juni Mosi baada ya kusimama kwa miezi miwili kutokana na janga la virusi corona.

Mingange alisema tangu walivyoanza mazoezi Jumatatu amefurahishwa na jinsi wachezaji wake wanavyopambana kuonyesha kuwa walikuwa wakifanya mazoezi binafsi wakati ligi iliposimama.

"Wachezaji wangu wote wamerejea na wana afya nzuri na nimeangalia kiwango cha kila mmoja  mazoezini na karibu asilimia kubwa wako vizuri hivyo inaonyesha walikuwa wanafuata kweli programu zangu walipokua nyumbani.

"Tunaendelea na mazoezi na tayari nimeshaongea na kocha wa Namungo (Thierry Hitimana) ili tucheze nao  mechi ya kirafiki ambayo itatusaidia kuziimarisha timu zote mbli kabla ya kurejea katika mikikimikiki ya ligi na amekubali hivyo nafikiri mwishoni mwa wiki tunaweza kucheza "amesema Mingange.

Advertisement


Advertisement