Nchimbi atangaza vita mpya na Kagere

Muktasari:

Nchimbi ana mabao matatu, ambayo aliyafunga kwenye mchezo dhidi ya Yanga huku Kagare akiongoza orodha ya wafungaji akiwa na mabao saba.

NYOTA wa Polisi Tanzania, Ditram Nchimbi anaamini anaweza kumzidi kete mshambuliaji wa Simba Mnyarwanda, Meddie Kagere na kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara kama akicheza msimu mzima bila ya kupata majeraha.

Nchimbi ambaye aliisaidia Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani CHAN 2020, anaamini kuwa mfungaji bora sio lazima uchezee klabu za Simba na Yanga.

“Naweza kuwa mfungaji bora hata kama naichezea Polisi Tanzania.

“Kikubwa ninachoomba ni kutopata majeraha, nikiendelea kuwa fiti, sidhani kama inashindikana hilo pamoja ya na ushindani ni mkali sana. Wapo washambuliaji wengi wanafanya vizuri,” alisema Nchimbi.

Aliendelea: “Hayo ni malengo binafsi lakini kitu muhimu zaidi ni kuhakikisha naisaidia timu yangu kumaliza msimu nafasi nne za juu kwenye ligi.”

Nchimbi ana mabao matatu, ambayo aliyafunga kwenye mchezo dhidi ya Yanga huku Kagare akiongoza orodha ya wafungaji akiwa na mabao saba.

Mchezaji huyo wa zamani wa Azam, tangu alipofunga Yanga ameshindwa kufunga katika michezo miwili iliyopita ya ligi dhidi ya Singida United timu yake ilishinda 2-1 , Oktoba 20 na dhidi ya Mwadui.