Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Refa wa 2-0 kuamua RS Berkane V Simba

REFA Pict
REFA Pict

Muktasari:

  • Simba imetinga fainali baada ya kuitoa Stellenbosch ya Afrika Kusini katika nusu fainali kwa ushindi wa bao 1-0 kupitia mechi mbili na sasa inakutana na RS Berkane ya Morocco iliyoitoa CS Constantine ya Algeria kwa jumla ya mabao 4-1.

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF), limemteua mwamuzi wa kati, Pierre Ghislain Atcho kutoka Gabon kusimamia mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho kati ya wenyeji, RS Berkane ya Morocco dhidi ya Simba kutoka nchini Tanzania.

Simba imetinga fainali baada ya kuitoa Stellenbosch ya Afrika Kusini katika nusu fainali kwa ushindi wa bao 1-0 kupitia mechi mbili na sasa inakutana na RS Berkane ya Morocco iliyoitoa CS Constantine ya Algeria kwa jumla ya mabao 4-1.

Simba itaanza kampeni za kusaka taji hilo kubwa Afrika kwa kucheza fainali ya kwanza ugenini Mei 17 ikiwa Morocco, kisha baada ya hapo itarudi jijini Dar es Salaam kwa mechi ya marudiano itakayopigwa Mei 25, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa huku kombe likiwa uwanjani.

Atcho anakumbukwa zaidi na Simba, kwani aliwahi kuchezesha mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, ambayo timu hiyo ya Msimbazi ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco, Desemba 19, 2023.

Mwamuzi huyo aliyezaliwa Oktoba 10, 1992, rekodi zinaonyesha amechezesha mechi 24 za kimataifa, ambapo timu za nyumbani zimeshinda 12, za ugenini zikishinda saba na tano zilizobakia zikiisha sare, akitoa kadi za njano 101 na nyekundu moja.

Atcho atasaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja, Boris Marlaise Ditsoga wa Gabon, msaidizi namba mbili ni Eric Ayimavo Ayamr Ulrich wa Benin, huku refa wa akiba mezani atakuwa Patrice Tanguy Mebiame wa Gabon.

Kwa upande wa Teknolojia ya Video Assistant Referee (VAR), katika mechi hiyo itaongozwa na Abongile Tom wa Afrika Kusini akishirikiana na Maria Packuita Cynquela Rivet wa Mauritania, huku msaidizi wa pili ni Diana Chikotesha kutokea Zambia.

Simba inaingia katika mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu mbaya mara ya mwisho ilipocheza ugenini dhidi ya RS Berkane kwenye hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika, ambapo timu hiyo ya Msimbazi ilichapwa mabao 2-0, Februari 27, 2022.

Baada ya kichapo hicho, Simba ikalipiza kisasi katika mechi ya marudiano iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa kushinda kwa bao 1-0, Machi 13, 2022, lililofungwa na aliyekuwa kiungo wa timu hiyo raia wa Senegal, Pape Ousmane Sakho.

RS Berkane, inasaka taji hilo la Afrika kwa mara ya tatu baada ya kuchukua msimu wa 2019–2020, ilipoichapa Pyramids ya Misri bao 1-0 na msimu wa 2021–2022, ilipoifunga Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwa penalti 5-4, baada ya sare ya 1-1.

Kwa upande wa Simba inasaka taji hili kwa mara ya kwanza ikiwa inashiriki fainali ya michuano hii kwa mara ya kwanza.

Fainali pekee ya Afrika ambayo Simba imewahi kucheza ni ya Kombe la CAF mwaka 1993, ambapo ilifungwa 2-0 na Stella Club d'Adjame ya Ivory Coast. Michuano hiyo ilikuja kuunganishwa na Kombe la Washindi na kuzaliwa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2004.

Katika fainali ya mwaka 1993, Simba mechi ya kwanza ugenini ilitoka suluhu (0-0), huku mashabiki wa kikosi hicho wakiwa na matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa, waliduwazwa nyumbani baada ya kuchapwa mabao 2-0, mabao ya Boli Zozo.