Nchimbi awaibua makocha Ligi Kuu

Dar es Salaam. Ditram Nchimbi alipoitwa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ kwa mara ya kwanza baadhi ya mashabiki walinyoosha kidole kwa kocha Etienne Ndayiragije.

Idadi kubwa ya mashabiki walidai Ndayiragije anachagua wachezaji kwa kufuata upepo na si ubora wa mchezaji huku wakimtolea mfano Nchimbi ambaye alifunga mabao matatu dhidi ya Yanga kabla ya kuitwa Taifa Stars.

Nchimbi alifunga mabao hayo katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao Yanga na Polisi Tanzania zilitoka sare 3-3 Oktoba 3, mwaka huu.

Wadau wengi na hata pengine makocha wa timu ya Taifa hawana rekodi ya Nchimbi kwani msimu uliopita alifunga mabao manane kwenye Ligi Kuu na kutoa pasi tisa za mabao.

Nchimbi ni ingizo jipya lililoibeba Taifa Stars dhidi ya Sudan na kuipeleka Fainali za Kombe la Mataifa Afrika Kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) zitakazofanyika mwakani, Cameroon.

Mchezaji huyo alifunga bao la pili akimalizia pasi ya Shabani Chilunda na ndiye aliyesababisha bao la kwanza lililofungwa kwa mpira wa faulo na Erasto Nyoni.

Taifa Stars ilishinda mabao 2-1. Nchimbi alifunga bao hilo muhimu akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Chilunda aliyekimbia na mpira na kuingia ndani ya eneo la adui kabla ya kupiga pasi iliyounganishwa vyema na Nchimbi.

Taifa Stars imekuwa na tatizo la muda mrefu la ubutu wa safu ya ushambuliaji jambo lililowapa hofu makocha na baadhi ya wadau.

Katika mechi tano za kufuzu Chan na Kombe la Dunia kabla ya mechi dhidi ya Sudan, safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars ilikuwa imefunga mabao mawili.

Mechi ya raundi ya kwanza kuwania ya Chan dhidi ya Kenya ilitoka suluhu nyumbani na ugenini na ilishinda kwa penalti 4-1.

Katika mchezo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022 dhidi ya Burundi ilitoka sare ya bao 1-1 ugenini na nyumbani na kusonga mbele kwa ushindi wa penalti 3-0 kabla ya kufungwa bao 1-0 nyumbani na Sudan.

Kauli za makocha

Kitendo cha Nchimbi kucheza kwa kiwango bora na kuibeba Taifa Stars limewaibua baadhi ya makocha ambao wanaamini Tanzania ina wachezaji wengi wenye vipaji ambao wanaweza kuibeba timu hiyo.

Kocha Kenny Mwaisabula alisema Nchimbi ameonyesha namna mchezaji yeyote akiaminiwa anaweza kuibeba nchi yake katika mchezo wowote.

“Nchimbi ameonyesha jinsi wachezaji ambao hawana majina wakiaminiwa wanaweza.

Huwa tuna tatizo kubwa katika uchaguzi wa wachezaji katika kikosi cha Stars mara nyingi wanaitwa kwa kuangalia wanatoka katika timu zenye mashabiki wengi na kongwe.

“Lakini ukizunguka katika timu nyingi hasa za mikoani kuna wachezaji wazuri ambao kama wakiaminiwa wanaweza kuibeba timu ya Taifa na kufanya maajabu kama ilivyokuwa kwa Nchimbi. Pia angalia hata Bakari Mwamnyeto wa Coastal Union alivyoziba pengo la Kelvin Yondani,”alisema Mwaisabula aliyewahi kuinoa Yanga.

Kocha wa JKT Tanzania, Abdallah Mohammed alisema timu ndogo zina wachezaji bora wanaoweza kuibeba timu ya Taifa, hivyo makocha wa timu hiyo wanapaswa kuanza kuangalia hilo.

“Tumeona Nchimbi alivyofunga goli lililotupeleka Chan na hiyo iwafungue macho makocha wa timu ya Taifa kuwa hata timu ndogo zina wachezaji wazuri na wenye vipaji wanaoweza kuibeba timu hiyo wasiangalie timu kubwa,”alisema Mohammed.

Kocha wa Prisons Mohammed ‘Adolf’ Rishard alisema licha ya kwamba janga la washambuliaji Tanzania ni kubwa lakini bado kuna wachezaji wengi ambao wakiaminiwa wanaweza kufanya vizuri timu ya Taifa.

“Kweli kuna tatizo kubwa la washambuliaji lakini hilo haliondoi uhalisia bado kuna timu nyingi kwenye Ligi Kuu zina washambuliaji hodari ambao wakipewa mazoezi na wakaaminiwa wanaweza kuwa msaada kwa Taifa na si lazima wote watoke timu kubwa,”alisema Rishard.

Fainali Chan

Taifa Stars imetinga Fainali za Chan zitakazofanyika mwakani nchini Cameroon lakini ikiwa na kazi kubwa mbele yake ili isirudie makosa iliyofanya mwaka 2009 nchini Ivory Coastal.

Mwaka 2009 Taifa Stars ilipofuzu Chan ilipangwa Kundi A na Zambia, Senegal, Ivory Coast.

Taifa Stars ilianza kwa kupata kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Senegal, ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ivory Coast kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 na Zambia.

Wakati huo huo, Katika mechi za Ligi Kuu zilizochezwa jana, Coastal Union ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Mwadui, Biashara United ilishinda 2-0 ilipocheza na Mbeya City wakati Polisi Tanzania iliichapa Singida United 2-1.