Namungo wamzuia Lusajo, Yanga

Muktasari:

Mwenyekiti wa Namungo FC, Hassan Zidadu alisema; “Hizo taarifa tunazisikia lakini hadi sasa hakuna ofa iliyokuja rasmi. Wachezaji wote hao wanaotajwa wana mikataba na Namungo na suala la kuwaongezea mipya ndio liko mezani kwa sasa ili waendelee kuitumikia timu yetu kwa muda mrefu zaidi.

NAMUNGO FC imesikia kuwa mshambuliaji wake Reliants Lusajo ameshaanza mazungumzo na Yanga ili ajiunge nao katika dirisha kubwa la usajili na baada ya hapo imetoa angalizo ambalo lisipofanyiwa kazi, mchakato huo huenda ukaota mbawa.

Klabu hiyo imeitaka Yanga na timu nyingine yoyote ambayo itamtaka Lusajo, iwafuate mezani na kumalizana nao kabla ya kufanya jambo jingine lolote kwa vile straika huyo aliyepachika mabao 11 kwenye Ligi Kuu hadi sasa msimu huu ana mkataba halali wa kuitumikia Namungo FC.

Mwenyekiti wa Namungo FC, Hassan Zidadu alisema; “Hizo taarifa tunazisikia lakini hadi sasa hakuna ofa iliyokuja rasmi. Wachezaji wote hao wanaotajwa wana mikataba na Namungo na suala la kuwaongezea mipya ndio liko mezani kwa sasa ili waendelee kuitumikia timu yetu kwa muda mrefu zaidi.

“Tutakuwa tayari kumruhusu aondoke lakini ni lazima taratibu zifuatwe kwa klabu husika inayomhitaji mchezaji kukutana na sisi na kufanya mazungumzo na tukifikia makubaliano basi tutamruhusu aende lakini kama watakuwa tayari kubakia, tutawaongezea mikataba,” alisema Zidadu.

Kwa upande wa Lusajo, alisema; “Kwa sasa kipaumbele cha kwanza kipo kwa timu yangu ila kama kuna timu inanihitaji, ni vyema iwasiliane na uongozi.” Mwanaspoti linajua kwamba anazuga tu kwani tayari ameshapokea simu za viongozi kadhaa lakini hawajafikia muafaka.

Mbali na Lusajo, nyota wengine wa Namungo FC ambao wanatajwa kuzitoa udenda Simba, Azam na Yanga ni beki Miza Christom, winga Hashim Manyanya, kiungo Lucas Kikoti na mshambuliaji Blaise Bigirimana.

Kiwango bora kilichoonyeshwa na wachezaji hao msimu huu kimekuwa gumzo kutokana na mchango mkubwa ambao wamekuwa wakiutoa kwa timu hiyo katika mashindano mbalimbali inayoshiriki.

Katika msimamo wa Ligi Kuu, Namungo FC iko nafasi ya nne ikiwa na pointi zake 50 ilizokusanya baada ya kucheza mechi 28 na pia imetinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Azam Sports Federation.

Kocha wa timu hiyo, Hitimana Thiery ameusisitiza uongozi kuhakikisha wachezaji wote muhimu kikosini wanasalia.