Namba hazisomi, rekodi za Arteta huko Arsenal majanga

LONDON, ENGLAND. MIKEL Arteta? Bora Unai Emery. Ndicho unachoweza kusema kuhusu mwenendo wa Arsenal kwa sasa huku takwimu zikifichua kila kitu hadharani.

Ni hivi, wakati Arteta akionekana kuanza kwa kasi kwenye ajira yake ya kuinoa Arsenal, lakini rekodi zake ni mbovu kuliko za mtangulizi wake, Emery.

Arsenal walifurahi kumpa ajira mchezo wao wa zamani Arteta majukumu ya kuinoa timu hiyo, lakini matokeo yao ya uwanjani hayajaonyesha tofauti yoyote kubwa kuliko Emery, huku hali ikionekana kuwa mbaya zaidi.

Kwa takwimu za makocha hao, Arteta na Emery baada ya mechi zao 38 za kwanza katika kikosi hicho, bosi wa zamani wa Paris Saint-Germain ameonekana kuwa bora zaidi.

Kwa rekodi za michuano yote, Emery ameshinda mara 23 dhidi ya 21 za Arteta na Arsenal yake imefunga mabao mengi, 74 dhidi ya 58 ya Arteta.

Kwa rekodi ya mechi 26 za mwanzo walizoongoza timu hiyo ya Arsenal kwenye Ligi Kuu England, Arteta rekodi yake imekuwa mbaya zaidi.

Akiwa ameaminika na kukabidhiwa mikoba ya kuinoa Arsenal kwa sasa, Arteta ameshinda mechi 12 tu kwenye Ligi Kuu, wakati Emery alishinda 15, huku Arteta amechapwa mechi nyingi, huku ikifunga mabao 40 huku ile ya Emery ilifunga mabao 53.

Chini ya Arteta, Arsenal imepiga mashuti machache sana na imekuwa na wastani wa hovyo wa kutikisa nyavu kupitia mabao hayo. Kipigo cha Jumapili iliyopita kutoka kwa Leicester City kimetibua zaidi rekodi za Arteta kwenye kikosi hicho cha Emirates.

Kwenye ligi, Arsenal ya Arteta imepiga mashuti 247, wakati ile ya Emery ilipiga mashuti 317. Kitu ambacho Arteta amekifanya cha maana kwenye kikosi cha Arsenal ni kuimarisha tu safu ya ulinzi, ambayo imeruhusu mabao 12 pungufu ya ile ya Emery katika mechi 38 za michuano yote. Arsenal hii ya Arteta imefungwa mabao 35, wakati ile ya Emery ilifungwa 47. Kwenye ligi, Emery alikuwa na wastani wa ushindi wa asilimia 57.6, wakati Arteta ana ushindi wa wastani wa asilimia 52.1.

Gwiji wa Arsenal, Martin Keown amemwambia Arteta aache kubadilibadili fomesheni kitu ambacho kimekuwa kikiiharibia timu hiyo na kupata matokeo ya hovyo yanayozidi kuzua maswali.