Mwl Kashasha sasa atabiri mfungaji bora

Saturday September 12 2020

 

Nianze kwa kusema tu kwamba msimu kwa sababu ndio umeanza, yako mambo mengi ambayo mtu unawezaa ukatakiwa kuyafikiria na kuyatafakari kuelekea nini kitatokea

Lakini tunajua kwamba lengo kubwa la timu yoyote kwenye mashindano hasa ya Ligi Kuu huwa ni kupata ubingwa.

Na ili kupata ubingwa, kila timu inahitaji kuwa na washambuliaji ambao ni mahiri, washambuliaji ambao watatumia nafasi zinazopatikana kulingana na mfumo na maandalizi yao.

Japo tunajua safari hii maandalizi hayakuwa marefu kiwango kile kutokana na janga la Corona lakini timu zimejibanabana hivyo wiki mbili wiki tatu, KMC wamekuwa na advantage naona wao waliona mbali zaidi na kama hawakupumzika vile.

Lakini all in all timu zote zinahitaji kupata mabao ili kupata ubingwa lakini pia ziweze kubaki Ligi Kuu, kinyume na pale zitakuja kupata idadi ndogo ya mabao ambayo itadetermine idadi ya points na mwisho wa siku timu zinakwenda kucheza play offs wengine wanateremka straighforward bila kucheza mechi za hatua ya mchujo.

Kwa hiyo kwa haraka naweza nikafikiria wachezaji wa wafuatao ambao huenda kwa sababu mbalimbali wanaweza wakawa kwenye orodha ya wachezaji saba wanaoweza kufanya mambo makubwa iwapo tu wataendelea kujituma kama tunavyowafahamu au rekodi zao zilivyo.

Advertisement

Wa kwanza ninayemuona anaweza kuchomoza na kuibuka mfungaji bora ni nahodha wa Simba, John Bocco. Bocco ameweza kuwa katika kiwango bora katika siku za hivi karibuni kutokana na uwezo wake wa kufumania nyavu na hata kupiga pasi za mwisho.

Katika mfumo wa kocha wa Simba wa kutumia striker mmoja, Bocco ameonekana kufiti vyema na amekuwa akioffer majukumu mengi ndani ya uwanja na sio jambo la ajabu kuona akianza kwa kuifungia Simba mabao mawili katika mechi mbili mfululizo walizocheza moja ikiwa ni ile ya Ngao ya Jamii dhidi ya Namungo waliyoibuka na ushindi wa mabao 2-0 na nyingine ni ile ya kwanza katika Ligi waliyopata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu.

Ukiondoa Bocco, mchezaji mwingine ninayemuona na ananipa imani kwamba anaweza kufanya vyema katika kufunga mabao ni Michael Sarpong wa Yanga.

Ni mzuri wa kucheza aerial balls, ana good positioning, anapiga mashuti, ana kasi na pia anatumia vizuri umbo lake na tayari ameshafunga bao moja katika mechi yake ya kwanza.

Kuna mchezaji ambaye kwa sasa hapati nafasi katika kikosi cha Simba lakini mimi namuona bado ni tishio naye ni Medie Kagere. Ana nidhamu ya nje na ndani ya uwanja, ana utulivu mbele ya lango lakini ana rekodi nzuri ya kufunga mabao zaidi ya 20 kwa kila msimu kwa misimu miwili aliyocheza hapa nchini ambayo pia amekuwa mfungaji bora.

Mchezaji mwingine ni Obrey Chirwa wa Azam. Huyu ana uzoefu wa ligi na ana uwezo mkubwa wa kufumania nyavu na pia ni mpambanaji asiyechoka ndani ya uwanja na usajili ambao timu yake imeufanya kwa kuwaleta akina Ayoub Lyanga na Prince Dube ambao wanajua kuchezesha timu, anaweza kufunga idadi kubwa ya mabao.

Pale KMC kuna Reliants Lusajo ambaye amesajiliwa na timu hiyo kutokea Namungo FC ya Lindi. Ni mchezaji ambaye amekuwa na muendelezo mzuri wa ubora akifunga mabao 11 katika Ligi Daraja la Kwanza kwenye msimu wa 2018/2019 na msimu uliopita akapachika mabao 12 na ni mzuri wa mipira ya juu na ya chini jambo linaloweza kumbeba.

Yupo winga wa Yanga Tuisila Kisinda. Ana kasi, chenga na utulivu wa hali ya juu pindi anapoingia katika lango la adui na ikiwa ataweza kutunza kiwango chake, huenda akaibuka mfungaji bora.

Mchezaji wa saba ambaye namuona anaweza kufanya jambo kubwa msimu huu katika ufungaji ni Blaise Bigirimana wa Namungo FC. ana uzoefu wa ligi, anajua kukaa kwenye nafasi sahihi kwa haraka na ni mwepesi kunusa hatari langoni mwa adui.

pamoja na hao saba, naweza kumuweka nyongeza mshambuliaji wa Kagera Sugar, Mbaraka Yusuf kwani ana akili ya kufunga mabao, ana uwezo wa hali ya juu kusoma mikimbio ya mabeki na pia ana utulivu.

Advertisement