Mwenyekiti aeleza alivyobaini kifo cha Mwangata

Muktasari:

Mwangata ameichezea timu ya taifa ya ngumi kwa mafanikio baada ya kutwaa medali ya fedha michezo ya Afrika, ameshiriki mara mbili Olimpiki tangu 1988 na michezo ya Jumuiya ya Madola kabla ya kustaafu na kuwa kocha wa timu ya Taifa sanjari na kuinoa klabu ya ngumi ya JKT.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Serikali za mtaa, David Chuma amesema waliingia ndani na kumkuta Benjamin Mwangata amefariki baada ya kutoonekana kwa siku mbili.

Mwangata bondia bingwa wa zamani wa michezo ya Afrika alikutwa amefariki ndani ya nyumba yake Jumapili asubuhi.

"Nilipigiwa simu ni diwani ambaye alipata taarifa hizo kupitia kwa rafiki wa karibu wa Mwangata aliyefika nyumbani kwa marehemu na kubaini kuna tatizo, nilipokwenda  tulikuta mlango wa sebuleni huko wazi lakini madirisha yamefungwa," alisema Mwenyekiti huyo wa mtaa wa Ulongoni A.

Alisema mlango wa chumbani ulikuwa umefungwa, waliuvunja na kuingia chumbani ambako walimkuta Mwangata akiwa amelala kitandani miguu ikiwa chini kana kwamba mtu aliyekuwa amejiegesha lakini tayari amefariki.

"Tulitoa taarifa polisi ambako walimchukua kwa uchunguzi na walipompekua walimkuta na vitambulisho, ingawa baadae tuliambiwa alifariki kwa kukosa hewa," alisema Mwenyekiti huyo.

Mwili wa Mwangata umeagwa leo nyumbani kwake na kusafirishwa kuelekea Mtwara kwa mazishi ambayo yatafanyika kesho Alhamisi.

Kaka wa Marehemu, Magnus Mwangata alisema wakati mauti inamkuta ndugu yao familia yake haikuwepo nyumbani.

"Walikwenda kusherehekea sikukuu ya Eid Jumatano kwa mmoja wa vijana wake, Kibaha, Mwangata alirejea nyumbani Alhamisi akaicha familia kule," alisema.

Mke wa marehemu, Ursula Mwangata alitumia dakika tano kumuaga mumewe ambapo alimuaga kwa kulifuta jeneza lenye mwili wa mumewe kwa kutumia khanga.