Mashabiki Mwanza mzuka mwingi baada ya ligi kuchezwa nyumbani na ugenini

Monday June 1 2020

 

WAKATI mechi za Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na la pili zikichezwa nyumbani na ugenini,mashabiki wa soka mkoa Mwanza wamefurahishwa na uamuzi huo wa serikali huku wengi wakifurahi kuona wataruhusiwa kutazama burudani hiyo.

Tangu mwezi machi mwaka huu michezo yote ilisimama baada ya serikali kupiga marufuku mikusanyiko kutokana na kuwepo kwa maambukizi ya virusi vya corona vilivyoingia nchini.

Hata hivyo baada ya Rais Magufuli kuruhusu michezo kuendelea,Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo,Dk Harrison Mwakyembe alitangaza ligi hizo kuchezwa katika kituo cha Dar es salaam na Mwanza.

Lakini  juzi Katibu wa Wizara hiyo na Msemaji mkuu wa Serikali,Hassan Abbas alitangaza michezo kuendelea huku ligi zitachezwa kwa mtindo wa kawaida huku mashabiki wakiruhusiwa kwa utaratibu maalumu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mashabiki hao walisema kwanza wamepata faraja kuona ligi hizo zitachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini na pia wao kuruhusiwa kutazama mechi hizo.

Lushinge Maboringo alisema wao burudani yao kubwa ni mchezo huo hivyo amefurahi kuona wameruhusiwa kutazama mechi hizo kwani mwanzoni walikosa raha kwani waliona fika wataishia kuona michezo hiyo kwenye runinga.

Advertisement

“Sie wengine ikifika jioni burudani yetu kubwa kwenda pale Kirumba au Nyamagana kwenda kutazama soka sasa tulikosa raha baada ya kuona hatutoweza kupata nafasi hiyo lakini tumefarijika kuona nasi tumeruhusiwa,” alisema Maboringo.

Shabiki Haruna Maregesi alisema kikubwa sasa baada ya wao kuruhusiwa ni kuhakikisha wanafuata taratibu za afya za kujikinga na ugonjwa huo huku wakitazama burudani hiyo ya soka.

“Ni jambo la kuishukuru sana serikali wameona sisi wengine starehe zetu ni kuja viwanjani kutazama soka ila niwaombe mashabiki wenzangu tuzingatie sana maelekezo tuliyopewa na wataalamu wa afya kwani bado maambukizi ya corona yapo,”alisema Maregesi.

Kocha wa zamani wa Toto Africans na mdau wa soka jijini Mwanza,John Tegete alisema kwake ana furaha tele kwanza kuona ligi zitachezwa kwa mtindo ule ule wa nyumbani na ugenini na pia mashabiki kuruhusiwa kuingia viwanjani.

“Kama ligi zingechezwa kwa vituo na pia mashabiki kutoruhusiwa kabisa basi mashindano yasingekuwa na mvuto lakini sasa serikali yetu ikaona mashindano yachezwe kwa mtindo uliopo ni jambo la kupongezwa,”alisema Tegete.

Advertisement