Yanga yazitaka pointi kwa KMC kupanda tano bora Ligi Kuu Tanzania

Monday December 2 2019

Mwanaspoti-Yanga-yazitaka-pointi-KMC-Tanzania-kupanda-tano-bora-Ligi-Kuu-Tanzania

 

By THOBIAS SEBASTIAN

WAKATI aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ikielezwa huenda leo akakutana na mabosi wake wa zamani ili kumalizana jumla baada ya kumtimua, lakini jioni pale Uwanja wa Uhuru, jeshi lake la zamani litakuwa na kazi kuwakabili KMC katika Ligi Kuu Bara. Lakini, kubwa kwa mashabiki wa klabu hiyo ni kutaka kuiona timu yao ikitinga Tano Bora kwa mara ya kwanza.
Yanga inahitaji pointi tatu tu ili kuingia Tano Bora kwa mara ya kwanza kwa kuichomoa Mtibwa Sugar waliotinga hivi karibuni baada ya kuichapa Kagera Sugar kwa mabao 3-1 mjini Bukoba.
Yanga itashuka uwanjani kwa mara ya nne ikiwa chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Charles Mkwasa, huku nyota wake  wakiongozwa na straika David Molinga na Patrick Sibomana wakiachiwa kazi ya kusaka pointi kabla ya kuvaana na watani zao, Simba.
Molinga ndiye kinara wa mabao Yanga akifunga manne, akifuatiwa na Sibomana mwenye matatu, wote wawili wakifunga mechi iliyopita dhidi ya Alliance na kuipandisha timu kutoka nafasi ya 15 hadi ya 12 na kama wataichapa KMC watatinga Tano Bora. Yanga chini ya Mkwasa imecheza mechi tatu na kushinda dhidi ya Ndanda, JKT Tanzania na Alliance, huku nyota hao wawili wakionekana moto katika kupasia nyavuni na kama leo itashinda itakuwa rekodi kwa Mkwasa kwani, ataingiza Yanga ndani ya Tano bora kazi iliyomshinda Zahera kabla ya kutimuliwa. Zahera aliiacha Yanga ikiwa nafasi ya 17 ikicheza mechi nne na kushinda mbili, sare moja na kupoteza moja ikikusanya alama saba tu. Pointi hizo saba zimeshapitwa na Mkwasa katika mechi tatu zilizopita kwani katika mchezo dhidi ya Ndanda, ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Sibomana, ya pili dhidi ya JKT Tanzania ikishinda 3-2, mabao yalifungwa na Sibomana, Molinga na Juma Balinya kabla ya Molinga na Sibomana kurudia tena CCM Kirumba, Mwanza wakati Yanga ikishinda 2-1 dhidi ya Alliance. Kama itashinda, Yanga itafikisha pointi 19 na kulingana na timu za Mtibwa Sugar, JKT Tanzania na Namungo zilizotofautiana mabao ya kufunga na kufungwa na kuziengua mbili ili kutinga Tano Bora huku pia ikiwa na michezo mkononi.
Yanga imecheza mechi saba na kukusanya pointi 16 ikifunga mabao 11 na kufungwa saba, mabao yanayoweza kuongezekana leo kama itashinda dhidi ya KMC na kumchomoa Mtibwa ambayo imefunga mabao 13 na kufungwa 12, lakini kwa kasi waliyoanza nayo chini ya Mkwasa ni wazi KMC ijipange, licha ya ukweli hata wao wanahitaji ushindi kujitoa mkiani.
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema timu yao itawakosa nyota wanne kutoka Zanzibar wakiwamo Feisal Salum, Abdulazizi Makame na Ali Ali waliopo kambi ya timu ya taifa ya Zanzibar inayojiandaa na Kombe la Chalenji linalooanza Jumamosi hii nchini Uganda. KMC leo watakuwa na kibarua cha kuhakikisha wanawachunga nyota hao wa Yanga hasa wakizingatia msimu huu hawana matokeo mazuri licha ya kumtimua kocha wao, Jackson Mayanja. Pia KMC wanaangusha na rekodi yao mbele ya Yanga, kwani katika mechi mbili za msimu uliopita zote walipasuka kwa vijana wa Jangwani, wakianza kufungwa 1-0 mchezo wa kwanza kwa bao la Feisal Salum, ambaye chini ya Mkwasa, amekuwa hana nafasi ya kucheza mara kwa mara. Katika mchezo wa marudiano, KMC walilala tena 2-1 kwa mabao ya Papy Tshishimbi na lingine aliyekuwa beki wao, Ali Ali alijifunga. Ali kwa sasa ni beki wa kati wa kikosi cha Yanga baada ya kusajiliwa msimu huu.
Mkwasa hakupatikana kuulezea mchezo huo, lakini nahodha Tshishimbi, alisema wamejiandaa wakipania kuendeleza rekodi ya ushindi na kuvuna pointi tatu.
“Mchezo utakuwa mgumu, lakini tumejiandaa kuwapa furaha mashabiki wa Yanga,” alisema kiungo huyo kutoka DR Congo. Licha ya KMC kuupania mchezo huo wa leo pia timu hiyo itakuwa ikitaka kuvuna ushindi wao wa tatu msimu huu, kwani katika mechi zao 10 wameshinda mbili na kupata sare mbili, wakipoteza sita na kushika nafasi ya 17 wakiwa ana alama zao nane tu. KMC inawategemea nyota wake kadhaa akiwamo Mu Ivory Coast, Serge Alain Nogues, Hassan Kabunda na Salim Aiyee alirejea upyaa.
Mbali na mechi ya Yanga na KMC, leo pia kuna mchezo mwingine wa kiporo wakati Biashara United chini ya Kocha Francis Baraza itaialika Ndanda kwenye Uwanja wa Karume, mjini Musoma, huku zikiwa hazichekani sana kwani zimetofautiana pointi nne tu.
Biashara ina pointi 12 wakati wageni wao wakiwa na nane zote zikiwa zimecheza mechi 12 kila mmoja, huku rekodi zinaonesha timu hizo zimekutana mara mbili zote kwenye ligi msimu uliopita na mechi ya kwanza Ndanda wakiwa nyumbani walishinda mabao 2-1, kabla ya Biashara kulipiza kisasi ugenini kwa kuwachapa wenyeji 2-0.

Kalengo kurudi
Katika hatua nyingine Bumbuli alisema straika wao Mzambia, Kalengo anatarajiwa kurejea nchini keshokutwa kabla ya Ijumaa kwenda kufanyiwa vipimo zaidi ili kujua afya yake.
Kalengo alirudi kwao kujiuguza na atarajea nchini Desemba 4, ingawa taarifa zinasema ni mmoja kati ya watakaoachwa kwenye dirisha dogo la usajili.

Advertisement